SANCHEZ SASA UHAKIKA KUCHEZA KAMA WINGA

TATIZO la kutokuwa na mshambuliaji halisi wa kati limeisumbua sana klabu ya Arsenal. Katika miaka ya hivi karibuni Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Arsene Wenger, amekuwa akihaha kusaka mshambuliaji wa kati bila mafanikio.

Alifikia hatua ya kuamini kwamba Alexis Sanchez angeweza kuwa mtu wake sahihi wa kupachika mabao akiwa kama namba 9. Sanchez, raia wa Chile, msimu huu ameanza mechi tatu za ligi kama mshambuliaji wa kati, lakini wakati huu hakuna namna, anatakiwa kuchezeshwa pembeni.
Wenger amemsajili fowadi wa Deportivo, Lucas Perez katika dakika za lala salama za dirisha la usajili wa majira ya kiangazi na namba 9 wao, Olivier Giroud anatarajiwa kurudi dimbani siku chache zijazo. Nafasi ya winga inamsubiri Sanchez.
Kilichomfanya Wenger aamini Sanchez angefanya vizuri mno kwenye eneo la kati, ni baada ya kukosa saini ya straika wa zamani wa Liverpool, Luis Suarez, mwaka 2013, ambaye kiuchezaji amefanana na Sanchez, lakini alipoona mambo magumu alimrudisha tena kama winga.
Msimu huu tena, Wenger alianza kwa kuwakosa Giroud aliyetoka kucheza michuano ya Euro 2016 na majeruhi Danny Welbeck, hapo akamtumia tena Sanchez eneo la kati kwenye michezo dhidi ya Liverpool na Leicester City, lakini hakung’aa kama ilivyotarajiwa.
Mshambuliaji wa kati mara nyingi hutakiwa kuwa na nidhamu kwenye eneo lake, awafanye mabeki kumwangalia yeye muda wote ili kutengeneza nafasi kwa wenzake.
Sanchez hawezi kutulia sehemu moja, ana njaa ya mpira na hilo linawapa tabu Arsenal, kwani wanaonekana kucheza bila kuwa na mlengwa pale mbele.
Ni mchezo mmoja tu dhidi ya Watford ndio walionekana kuwa na mlengwa, na hilo lilichagizwa na uwepo wa kiungo mbunifu, Mesut Ozil. Timu yoyote ikiwa na Ozil nyuma ya washambuliaji, ni lazima wataonekana ni watu hatari.
Lakini kwa sababu ameshatua Perez, Wenger hana budi kumtumia katikati ili ampe nafasi Sanchez ang’ae pembeni.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment