Video Queen Giggy Money: Asema Nyie chongeni tu mimi napiga hela



KITU kinachozifanya video nyingi za muziki mbalimbali kupendwa na mashabiki ni ubora wa uandaaji wake. Ubora huo huwa na vitu vingi ndani yake na moja ya vitu hivyo ni warembo wanaotumika kwenye video hizo.
Kwa lugha ya wenzetu wanawaita ‘video queens’.
Ni warembo ambao huwa ni kivutio kikubwa kwa mashabiki kutokana na madoido yao wakati wa kucheza miondoko ya wimbo husika na jinsi wanavyoongeza vionjo kitu ambacho huwafanya mashabiki wapate burudani ya kutosha.

Kwa hapa nchini, mmoja wa ‘video queen’ anayenogesha video za wasanii mbalimbali wa muziki ni mwanadada Gift Stanley ‘Giggy Money’ ambaye pia ni mtangazaji wa kipindi cha historia za mapenzi ‘malavidavi’ kinachorushwa na Redio Choice FM.
Kimwana huyo anayetesa kwenye video mbalimbali kwa sasa, hivi karibuni aliandamwa kwa maneno makali kwenye mitandao ya kijamii ambapo watu wamekuwa wakiziponda picha zisizo na maadili.
Ni nani huyu Giggy Money? Mwanadada huyo ni mtoto wa pili katika familia yao yenye watoto watatu, elimu yake ni ya kidato cha nne na mara baada ya kumaliza elimu yake hiyo alijikita katika masuala ya muziki ambapo moja kwa moja akawa ‘video queen’ kwenye nyimbo mbalimbali za wasanii wa Bongo ukiwemo wimbo wa ‘Niwachane’ wa Ney wa Mitego.
Kuhusu suala la kuandamwa na maneno makali kutoka kwa Watanzania, Giggy anafunguka kwa kusema yeye si muuza sura kwenye mitandao ya kijamii bali yupo kibiashara na kitu anachokifanya kinamwingizia fedha zaidi ya watu wanavyomfikiria.
Wakati watu wakimsema na kumponda kwa kile anachokifanya mrembo huyo, yeye mwenyewe akaendelea kufunguka: “Kuna aina nyingi tu za kutafuta fedha. Maisha magumu niliyopitia ndiyo yaliyonifanya nikaangalia ni njia gani nitumie ili nijikwamue kiuchumi.”
Anaongeza kwa kusema: “Huu mvuto nilionao ni kwa sababu ya fedha ninazozipata kutokana na kazi ninayoifanya. Sijawahi kukataa ninachokifanya kwani nakiamini sana.”
Watu wengi huwa wanamchukulia mrembo huyu kama mwanamke asiyejitambua lakini anasema yeye hawezi kufanya vitu vya ajabu bila faida bali hiyo ni kazi inayompa faida kubwa na anaiheshimu kama kazi nyingine.
Baada ya kufanya vizuri na kufanikiwa kujitangaza zaidi katika soko la sanaa, Giggy Money anazidi kuweka wazi kwa kusema maisha yake hayakuwa na mwelekeo unaoeleweka kwani aliwahi kuwa mtumiaji wa bangi na hilo lilitokana na makundi mabaya aliyoyafuata.
Mrembo huyo alisema aliamua kuachana na mkumbo huo kwani aliona umri unazidi kusonga na hali ya kimaisha inakuwa ngumu zaidi ndipo akili yake ilipoamka na kuanza safari mpya ya maisha yake.
“Safari yangu ya maisha ndio kwanza imeanza na mipango yangu ni kufika ‘levo’ za kimataifa niitangaze Tanzania japokuwa changamoto ninazokutana nazo ni nyingi.
“Watu wengi hawaitaki kazi yangu hii, wananichafua, nadharauliwa na kuonekana sifai katika jamii vitu ambavyo kwangu mimi nataka nivishinde ili kusonga mbele na maisha yangu.”
Kazi ya ‘u-video queen’ imemfanya Giggy kupata mafanikio mengine ya ziada ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba ya kutangaza nguo za ndani.
“Namshukuru sana Mungu kwani kazi hii imenipatia fursa nyingine za ziada. Matangazo ninayoshiriki yananiwezesha zaidi kiuchumi. Nakula vizuri, nalala sehemu nzuri na kutatua matatizo madogo madogo ya kimaisha,” anasema Giggy.
“Najiamini kuwa mimi ni mwanamke shupavu nisiye na muda kuzungumza ya watu na sifuatilii maisha ya yeyote. Ninamwamini muumba wangu na kila kitu nafanya kwa kumtegemea yeye hivyo binadamu hawawezi kunisumbua akili,” anaongeza mrembo huyo.
Ushauri anaoutoa Giggy kwa vijana ni kufanya kazi kwa bidii na kuacha ‘ubishoo’ usio na faida katika maisha kwani huu ni wakati wa kila mtu kufanya kazi ili kujikwamua kiuchumi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment