KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata amewaonya watumishi wa idara hiyo kutojihusisha na vitendo vya rushwa, vinginevyo atawachukulia hatua za kinidhamu na kuwaachisha kazi.
Kamishna huyo alisema hayo jana katika kikao cha watumishi wa idara hiyo mkoani Mara wakati akikagua kituo cha forodha katika eneo la Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kamishna Mkuu Kidata alisema, " Katika kituo hiki kuna watumishi zaidi ya 12 wanaotuhumiwa kujihusisha na hujuma kwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu, wafanya magendo wanaopitisha bidhaa za biashara zao kwa njia za panya, na watumishi wengine wanatuhumiwa kushirikiana na wafanyabiashara kuvusha malori ya bidhaa kwenda nchi jirani.
Meneja Msaidizi ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Forodha Sirari, Nircissius Moshi akisoma taarifa fupi kwa Kamishna huyo alisema, kituo chake kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za Jeshi la Polisi kwenye vituo vya mipakani kutotoa ushirikiano katika kudhibiti biashara ya magendo katika mipaka ya Sirari, Kogaja, Kubiterere, Borega na Shirati na nyingine ni jengo jipya la Forodha walimo sasa halina miundombinu ya mtandao wa intanet na hakuna mfumo wa maji, linavuja baadhi ya vyumba.
Meneja Msaidizi Moshi, alisema kuwa, " Mgodi wa Acacia North Mara unachangia kwa asilimia 75 katika ulipaji mapato katika kituo cha Forodha Sirari, tunatarajia kufanya vikao vya pamoja na semina na kuwashirikisha wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ili waweze kurejea kupitisha bidhaa zao katika kituo cha Sirari kufanya doria za pamoja na wenzetu wa Isebania, Kenya ili kuweza kupambana na biashara ya magendo kwani kuna njia nyingi za panya katika mpaka huu, " alisema Moshi.
Ofisa TRA wa Isebania nchini Kenya, Martin Otieno alisema, " Tunafanya vikao vya pamoja na wenzetu hawa wa upande wa Tanzania, ili kupambana na vitendo vya biashara za magendo ambazo zimeshamiri katika mipaka hii ya Isebania na Kenya na kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi bila shuruti kwa pande zote kwa manufaa ya nchi zetu, " alisema Otieno.
Blogger Comment