Kuahirisha Ukuta, Polisi Wapumua

JESHI la Polisi limepumua baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuahirisha mikutano na maandamano yao, anaandika Pendo Omary.

Hatua ya kuahirisha mikutano na maandamano iliyotangazwa kufanyika chini ya mwavuli wa operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta), imepongezwa na Simon Sirro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.


Kulikuwepo na vuta nikuvute kati ya Chadema na serikali kuhusu Ukuta hivyo kuzua taharuki na hisia za kutokea machafuko iwapo juhudi za kutafuta suluhu zingeshindikana.

Maandamano hayo yalitarajiwa kuanza kufanyika kesho lakini leo Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho ametangaza kusitisha kwa kile kilichoelezwa, uchaguri wa taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuisha mazungumzo ya taasisi hizo na Rais John Magufuli.

“Nawashukuru sana viongozi hawa kwa uzalendo waliouonesha kwa kusimamisha mikutano na maandamano yao.

“Ila kuhusu kesho, wananchi wasishangae kuona magari yetu yakipita barabarani wakajiuliza kulikoni wakati Chadema wametangaza kutoandamana. Sisi kama Jeshi la Polisi bado tupo kwenye oparesheni zetu za kupambana na wahalifu,” amesema Siro.

Aidha, Sirro amesema oparesheni inayoendeshwa na jeshi hilo katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam inaendelea vizuri na mpaka sasa tayari linawashikilia watuhumiwa zaidi ya 20 baada ya kufanya msako mkali.

“Watu zaidi ya 20 wamekamatwa. Wengi wanaeleza namna wanavyolifahamu tukio (mauaji ya askari wanne), lakini wengine ni wahusika katika matukio mengine ya uharifu. Ukamataji bado unaendelea katika maeneo ya Vikindu na Dar es Salaam,” amesema Sirro
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment