Mwenyekiti wa Taasisi inayoshughulikia masuala ya Afrika (Africa Matters Limited) Mhe. (Baroness) Lynda Chalker wa Wallasey - Uingereza, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa alizozifanya kupiga vita rushwa na kujenga mazingira bora zaidi kwa uwekezaji.
Mhe. Lynda Chalker ametoa pongezi hizo jana tarehe 31 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo hali ya uwekezaji hapa nchini.
"Mhe Rais amefanya uamuzi sahihi wa kupiga vita rushwa na kuiweka nchi hii katika njia mpya ya uwekezaji mzuri na hicho ndicho tumekuwa tukikizungumza, nimejitahidi kutoa ushauri wangu wa namna mimi na kampuni yangu binafsi tunaweza kumsaidia, nionavyo mambo yanakwenda katika mwelekeo mzuri" Amesema Mhe. Lynda Chalker.
Kwa Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Lynda Chalker kwa ushauri na dhamira yake ya kutaka Tanzania ipige hatua kimaendeleo na amemuomba kutumia ushawishi wake kuwahamasisha wawekezaji mbalimbali kutoka nchini Uingereza na kwingineko duniani kuja kuwekeza nchini Tanzania ili kuharakisha zaidi maendeleo.
Hata hivyo Dkt. Magufuli amesema wawekezaji wanaokuja Tanzania hawana budi kuwa wawekezaji makini.
"Ninawakaribisha wawekezaji makini kutoka Uingereza na mahali popote dunia, lakini nisingependa kupata wawekezaji wababaishaji" Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016
Blogger Comment