Na: Lilian Lundo- Maelezo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia watanzania kwamba mipaka ya Tanzania ni salama.
Mhe. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) alipokuwa akieleza mikakati ya wizara hiyo katika kuhakikisha mipaka ya Tanzania iko salama.
“Nchi iko salama, mipaka ya nchi iko shwari, ziko changamoto chache za nchi zinazotuzunguka kuwepo katika machafuko mfano Burundi hivyo wananchi wake kukimbilia Tanzania,” alifafanua Mhe. Dkt. Mwinyi.
Amesema Tanzania sio kisiwa, imejiunga na jumuiya mbali mbali kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa hivyo kupitia Jumuiya hizo Tanzania hupata maelekezo ya kuwapokea wakimbizi kutoka nchi zenye machafuko.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inahakikisha wakimbizi wanaoingia nchini wanafuata utaratibu unaotakiwa bila kuvunja sheria za nchi.
Pia ameeleza kuwa Tanzania inaendelea na mazungumzo ya amani na nchi ya Malawi juu ya mgogoro wa umiliki wa Ziwa Nyasa baina ya nchi hizo mbili ili kupata ufumbuzi wa amani, ambapo mazungumzo hayo ya yanaongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa kutokana na Wizara hiyo kufanya vizuri katika Ulinzi na Amani ya Nchi, Jumuiya ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa imeiomba nchi ya Tanzania kutoa Ulinzi wa Amani kwa nchi za Sudani, Kongo na Lebanoni kutokana na machuko yanayoendelea katika nchi hizo.
Vile vile ameeleza kuwa, ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika nchi zenye machafuko kunaisaidia Jeshi hilo kupata mafunzo ya kivita kutokana na Tanzania kuwa ni nchi ya amani hivyo kufanya baadhi ya wanajeshi kutoshiriki mafunzo ya uhalisia ya kivita tangu wanapoajiriwa mpaka kustaafu.
Blogger Comment