NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani amelitaka gazeti la Mseto kumuomba radhi na kumlipa fidia ya Sh bilioni moja kutokana na kuandika habari aliyodai ni ya kumchafua.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Ngonyani alisema gazeti hilo katika toleo lake la Agosti 4, mwaka huu liliandika habari yenye kichwa cha habari “Waziri amchafua JPM” ikimhusisha na upokeaji wa fedha kutoka moja ya kampuni ya madini wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
“Nimewaandikia notisi ya siku saba ikiwataka waombe radhi na kunilipa fidia na wasipofanya hivyo hatua stahiki kuwapeleka mahakamani akiwemo Mwandishi Josephat Isango, Mwanahalisi Publishers na Mchapaji wa gazeti hilo,” alisema.
Alisema habari hiyo siyo ya kweli na mwandishi ametumia nyaraka za kughushi ikiwemo barua iliyoandikwa Julai 24, mwaka huu na kutiwa saini yake akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Stamico wakati ukweli ni kwamba tarehe hiyo yeye alikuwa ni Mkurugenzi kamili na siyo Kaimu kama barua hiyo inavyosomeka.
Aliongeza kuwa, habari hiyo imewachafua watu wengi ikiwemo familia yake, wapiga kura wake wa Jimbo la Namtumbo ambao walijitoa katika kumsaidia wakati wa kampeni na hali kadhalika zimemchafua Rais John Magufuli kwa kumhusisha na fedha kutoka kwa wawekezaji wa nje kwa kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini itakuwa salama.
“Mheshimiwa Rais Dk Magufuli alishasema kama kuna mfanyabiashara yeyote aliyechangia kuingia kwake Ikulu ajitokeze na hakuna aliyefanya hivyo, iweje leo mtu tu anaibuka na kuandika habari za kughushi?” Aliongeza.
Blogger Comment