DAR ES SALAAM: Imevuja! Siku chache baada ya Mbongo Fleva, Emanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuhusu chanzo cha utajiri wake wenye utata, mwenzake katika fani, Nasibu Abdul ‘Diamond’ naye amekumbana na kimbembe cha kuchunguzwa na TRA, Amani lina kitu mkononi.
TRA ni Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo inajishughulisha na ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla ili kuiletea nchi maendeleo kutokana na pesa hizo za kodi.
Kwa mujibu wa chanzo, Diamond alikumbwa na kimbembe hicho mwaka huu kabla ya Nay na kwamba, jamaa wa TRA walimvamia nyumbani kwake, Madale na kutaka aorodheshe mali zake zote ili ambazo hazijalipiwa kodi zijulikane.
“Jamani, mmeandika habari za Nay kukamatwa na polisi na kuhojiwa kwa siku mbili kwa sababu ya utajiri tata. Sasa mimi nawaambia ubuyu mwingine kwamba, Diamond naye alishikwa na watu wa TRA, wakawa wanamhoji kuhusu mali zake zote.”
“Walianzia nyumbani kwake Madale, wakaangalia uhalali wa nyumba yake na vitu vingine kama magari na vyote ambavyo vinatakiwa kulipiwa kodi.”
“Baada ya kutoka Madale, walikwenda kwenye nyumba aliyoifanyia ukarabati, ile ya Tandale (Dar). Kule nako jamaa walifanya mahesabu yao, wanajua wenyewe walichokipata.”
“Baada ya Tandale, wakaona bado, wakaenda kwenye studio yake (Wasafi Records) iliyopo Sinza Mori, Dar, nako wakaangalia kila kitu kilichomo na uhalali wake kama havidaiwi kodi.”
NYUMBA ALIYONUNUA
“Kama vile haitoshi, wakaenda kwenye ile nyumba aliyonunua, iliyopo Salasala, Dar ambako pia waliipigia thamani na kuangalia kama alilipia kodi kwenye manunuzi.”
ILICHUKUA SIKU SABA
“Afadhali ya Nay alihojiwa kwa siku mbili, Diamond ni siku saba, sema tu yeye, jamaa wa TRA walikuwa wanambana mchana kutwa na kumwachia jioni,” kilisema chanzo hicho.
DIAMOND ACHANGANYA AKILI
Chanzo hicho kilisema kuwa, mwisho wa kumbana, Diamond aliambiwa anatakiwa alipie kodi kwa kila kitu ambacho alikwepa kufanya hivyo.
“Lakini jamaa (Diamond), akachanganya akili zake, akaamua kumtumia kigogo mmoja serikalini ambaye alimsaidia. Kigogo huyo aliwaambia watu wa TRA wamuachie kwa sababu utaratibu waliuharibu wenyewe tangu mwanzo kwa kuacha kukusanya mapato kwa uzembe. Ndipo Diamond akaachiwa,” kilisema chanzo.
‘KIAMA’ CHA MASTAA
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kilichompata Diamond na Nay ni mwendelezo wa kampeni ya serikali kuhakikisha mastaa wote wanaotamba na utajiri, wanalipa kodi na pia utajiri wao uwe halali huku wale wanaomiliki utajiri usio wa halali, wakitangaziwa mwisho wao (kiama)
Blogger Comment