SABODO AMSHAURI RAIS MAGUFULI AZIDI KUPUNGUZA BARAZA LA MAWAZIRI


 Mfanyabiashara maarufu nchini, Jaffar Sabodo akizungumza nyumbani kwake Upanga Dar es Salaam  mwishoni mwa wiki, ambapo alimtaka Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Rais John Magufuli azidi kupunguza Baraza la Mawaziri kufikia 15 na Kamati Kuu 15 pamoja na Halmashauri Kuu wajumbe 55.



MFANYABIASHARA maarufu nchini, Jaffar Sabodo, amemshauri Rais John Magufuli kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, akisema hali hiyo itamsaidia kuleta tija zaidi katika utendaji wake.

Aidha, Sabodo amemshauri Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMBO LEO nyumbani kwake Dar es Salaam, Sabodo alisema hatua hiyo itasaidia Serikali kutekeleza falsafa yake ya kubana matumizi.

“Kupungua kwa ukubwa wa Baraza la Mawaziri kutajenga uwajibikaji zaidi kwa mawaziri, lakini pia kubana matumizi ya Serikali kuhudumia baraza kubwa la mawaziri pia kusaidia kujenga mfumo imara zaidi wa utawala na itakuwa rahisi kudhibiti siri za Serikali,” alisema Sabodo na kuongeza:

“Hata ukubwa wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za CCM nao ukipungua utaiimarisha zaidi CCM, kwani viongozi wake watakuwa na nguvu zaidi, lakini pia matumizi yatapungua na mambo ya chama hayatavujishwa kirahisi.”

Alipoulizwa kuhusu idadi anayopendekeza iwe kwa vyombo hivyo, Sabodo ambaye amewahi kuwa mfadhili wa CCM na Chadema kwa nyakati tofauti alisema: “Ili kulinda zaidi maadili ya CCM yawe kama alivyoacha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyeiasisi, kwa mawazo yangu Halmashauri Kuu ingekuwa na wajumbe wasiozidi 55 na Kamati Kuu wawepo wajumbe wasiozidi 15.”

Kuhusu Baraza la Mawaziri Sabodo alisema linapaswa kupungua kutoka idadi ya sasa hadi kufikia mawaziri wasiozidi 15. “Cabinet’ baraza liwe dogo, kuna wizara zinaweza kufutwa, ili kuleta tija zaidi. Hili linawezekana,” alisema Sabodo.
Ushauri huo wa Sabodo umekuja wakati hivi karibuni CCM ilitangaza mabadiliko na kupunguza idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka 388 hadi 158 huku wajumbe wa Kamati Kuu ikipunguzwa kutoka 34 hadi 24.
Kwa upande wa mawaziri, Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli lina mawaziri kamili 20 pamoja na Waziri Mkuu, likiwa na naibu mawaziri 16.
Akizungumzia uamuzi wa Rais Magufuli kuhamia Dodoma, Sabodo alisema ameonesha uthubutu ulioshindikana kwa zaidi ya miaka 45.
Alisema anakumbuka uamuzi wa kuhamia Dodoma ulifikiwa na Bunge enzi za utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyeshindwa kuufanikisha kutokana na sababu mbalimbali za msingi, lakini waliofuata katika uongozi hakuna aliyeonyesha uthubutu kama wa Rais magufuli.
Sabodo alisema hatua hiyo ya kuhamia Dodoma ikifanikiwa inaweza kusaidia hata rushwa na ubadhirifu kupungua kwani baadhi ya mambo yatashindikana kufanyika Dar es Salaam litakalobaki kama jiji la kibiashara hivyo kuwalazimu wahusika kwenda makao makuu ya Serikali.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment