RAIS John Magufuli amewakataza mameya wa majiji, manispaa na halmashauri za miji, kuwatimua wamachinga katika maeneo ya katikati ya jiji na miji kabla ya kuboresha miundombinu mahali wanapotakiwa kufanyia biashara.
Rais alitoa katazo hilo akiwa ziarani mkoani Mwanza wakati akihutubia wakazi wa jiji hilo waliofurika viwanja vya Furahisha.Alirudia wakati akizungumza na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) waliofika kumpokea kwenye ofisi ndogo za chama hicho Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
Kauli ya Rais Magufuli imekuja baada ya kusikika kuwatimua wamachinga katika majiji, manispaa na halmashauri nyingi kwamba wanafanya biashara katika maeneo yasiyohusika kwa ajili yao. Rais Magufuli amesisitiza kwamba hakuna kuwaondoa wamachinga mjini kwani huko nje ya miji wanakopelekwa hakuna wateja, miundombinu ya kuwafanya wafanye biashara haipo.
Aliwataka mameya hao kuandaa miundombinu kwa ajili ya kuwarahisishia wamachinga hao kufanya biashara yao. Sisi tunaunga mkono kauli ya Rais Magufuli ya kutowatimua wamachinga katikati ya majiji au miji kabla ya kuwaandalia miundombinu ya kufanyia biashara zao.
Wafanyabiashara ndogo ni muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda, hivyo wanatakiwa kutobughudhiwa, kusumbuliwa na mgambo wa majiji kwa kufukuzwa, badala yake wasaidiwe kuandaa mazingira yao.
Sisi tunaunga mkono kauli ya rais kwani inaonesha nia ya dhati ya kuwasaidia wamachinga kufanya biashara katika maeneo yaliyotengwa na kuwekwa miundombinu. Wamachinga wakiandaliwa maeneo mahususi ya kufanyia biashara wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kuchangia pato la taifa na kukuza uchumi wa nchi.
Kauli ya Rais Magufuli inaonesha hapendi wamachinga kufanya biashara kila mahali, mfano pembezoni mwa barabara na mahali pengine pasipotakiwa, anachotaka ni viongozi wa maeneo husika, waandae mipango madhubuti ya kupanga majiji yao na kutenga maeneo ya wafanyabiashara ndogo.
Kinachotakiwa kutangulia ni kuandaa maeneo ya wafanyabiashara ambayo miundombinu ya barabara, maji, umeme na mingine imefikishwa mahali hapo. Kampeni ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogo kando ya barabara, nje ya maduka ya wafanyabiashara wengine, kwenye maeneo ya stendi za mabasi na maeneo mengine, yanatakiwa kufanyika baada ya kuboresha miundombinu kwenye maeneo hayo.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli pia imesisitizwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipotembelea ujenzi wa kituo cha mabasi Msamvu, Morogoro, Agosti 3, mwaka huu, ambapo aliwaagiza viongozi wa manispaa hiyo kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Pamoja na kutenga maeneo hayo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kuwasaidia wafanyabiashara hao kuunda vikundi kulingana na aina ya biashara wanazozifanya, ili kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi kutoka katika taasisi za fedha.
Sisi tunaunga mkono agizo la Rais Magufuli ambalo limesisitizwa na Waziri Mkuu, Majaliwa, kuandaa mazingira na miundombinu ya maeneo ya wafanyabiashara ndogo ndipo waondolewe kutoka katika maeneo mbalimbali ya majiji, manispaa na mijini, badala ya utamaduni wa sasa wa kuwatimua na kuwafukuza bila kuwaonesha wapi pa kwenda.
Blogger Comment