Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amekiri bunge hilo kusambaratika na kuwa vipandevipande kutokana na vurugu za mara kwa mara zilizopelekea wabunge wa upinzani kususia vikao hivyo anawaalika wabunge hao kwenye mazungumzo.
Ndugai, ambaye kipindi kirefu cha Bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni, alikuwa India kwa matibabu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Funguka kinachorushwa na televisheni ya Azam.
Ndugai alisema ili bunge lifanye kazi yake yake, linahitaji kuishinda changamoto iliyopo ya bunge kutokuwa kitu kimoja, huku akielezea wazi kuwa chanzo kikuu kinachosababisha bunge hilo kusambaratika ni pamoja na "u-vyama" kuzidi na wabunge kutojali maslahi ya taifa.
Sababu nyingine aliyoitaja Ndugai, ni ugeni wa wabunge ambapo kila unapofanyika uchaguzi sehemu kubwa ya wabunge huwa ni wageni hivyo wengi wao wanakuwa hawajaelewa kanuni na tamaduni za kibunge.
Alisema yanayotokea sasa kwa kiasi kikubwa siyo mageni, yalikuwepo tangu wakati wa bunge la 10.
"Hali hii imeanza zamani kidogo tangu enzi za spika Makinda, wabunge walikuwa wakitoka nje, wakigomea vikao, wakiadhibiwa n.k. Ugumu ambao tunaupata ni kwamba kila baada ya uchaguzi wanakuja wabunge wengi wageni ambao hawajui mambo mengi na mfano ni bunge hili ambapo karibu 70% ya wabunge ni wapya"Alieleza Ndugai na kuongeza kuwa hata suala la kumsusia Rais anapokwenda kuhutubia bungeni, limewahi kutokea katika bunge lililopita.
Pamoja na hayo, Spika Ndugai alisema kuwa hakuna kanuni inayomzuia mbunge kutoka nje ya bunge kwa kuwa ni haki yake
"Hakuna kanuni inayomkataza mbunge kutoka nje, ni sehemu ya demokrasia yao, lakini hii ya sasa imezidi, ni jambo lisilopendeza... maana watanzania wamewatuma kwenda kuwakilisha hoja zao, wanapotoka inakuwa haipendezi".
Aliwasihi wabunge wa Upinzani kurudi bungeni na kueleza mambo yaliyowaudhi ili wakae wajadili na watafute ufumbuzi badala ya kuendelea kususia.
Alisema "Wabunge kutoka nje ni jambo ambalo halipendezi hata kidogo, nisingependa niendelee kuliona.
"Nawaomba katika bunge lijalo kama wanahisi tunakosea watueleze, na sisi tuwaeleze wanakosea wapi ili twende sawa"
Kuhusu malalamiko ya wapinzani dhidi ya Naibu Spika, alikiri kupokea malalamiko hayo kupitia kwa mbunge james Ole Millya, na yeye aliyawasilisha kwenye kamati husika lakini hoja zote ambazo walikuwa wakizilalamikia zilizonekana hazina uthibitisho, hivyo maamuzi ni kwamba Naibu Spika Dkt Tulia Ackson hana hatia yoyote.
Kuhusu hoja ya Naibu Spika kuendelea kukalia kiti kwa muda wote Ndugai anasema " Uongozi ndiyo unapanga nani akae pale, sioni tatizo la mtu kukaa kwenye kiti kwa muda mrefu, lakini kama mtu anakosea, zipo fursa za kupeleka jambo kwenye kamati badala kulalamika bila kufuata kanuni"
Alisema haoni tatizo la Naibu Spika na hajui ni mambo gani amewaudhi ila anadhani kinachowasumbua wapinzani ni hisia za jinsi Naibu Spika alivyopatikana
"Wabunge wa upinzani wanapitia changamoto nyingi kabla ya kuingia Bungeni, wengi wao wanahangaika sana kupata ubunge hadi kufikia hatua ya kulala sana selo (polisi) kwaiyo namna ya 'kudeal' nao inahitaji uvumilivu kidogo. Naibu Spika siyo mbunge wa jimbo, na wao wamezoea mbunge wa jimbo ambaye anafanana nao, Naibu Spika ni mbunge wa uteuzi kwahiyo wanahisi anafanya kazi kwa kufuata maelekezo kutoka nje ya bunge au anatumikia mabwana wawili jambo ambalo siyo kweli. Pia adhabu zilizokuwa zinatolewa zinawafanya wahisi wanaonewa kila wakati"
Pia Spika alikemea tabia ya baadhi ya wabunge wa CCM kutumia muda mwingi bungeni kurusha vijembe kwa wabunge wa upinzani
"Kwa wabunge wa chama tawala siyo jambo zuri kurusha vijembe, tukienda bungeni nitakaa nao, na nitawaeleza kuwa siyo jambo jema kuwa na bunge la vijembe, nawaasa tubadilike, tuheshimiane ... matusi kelele vijembe kanuni haziruhusu na haipendezi"
Kuhusu mwenendo wa baadhi ya wabunge kutoheshimu kanuni, Ndugai alisema "Kanuni zimetungwa kwa watu wazima, lakini tatizo wabunge wanaokuja sasa hivi wengi ni vijana, na wako chini ya kiwango cha kanuni. Bado sijajua nini cha kufanya ili hali hii isiendelee, kwenye bunge la katiba angalau kulikuwa na kitu kinaitwa kamati ya maridhiano, nafikiri inabidi tuige kitu hicho tupate watu hata wastaafu watakaokuwa wanakaa kuyaweka mambo haya sawa"
Kuhusu sakata la Lugumi, Ndugai alisema kuwa kamati ndogo iliyoundwa kufuatilia suala hilo itatoa taarifa yake katika mkutano ujao wa bunge.
Kuhusu uamuzi wa serikali kuzuia Bunge LIVE, Ndugai alisema uamuzi huo ni mzuri na anauunga mkono kwa kuwa unasaidia kupunguza vurugu kwa wabunge.
Kuhusu suala la posho za wabunge Naibu Spika alisema kuwa posho za wabunge wanazolipwa sasa, ni za kawaida na siyo kubwa kama watu wanavyodhani huku akiunga mkono uamuzi wa wabunge kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo.
Blogger Comment