SERIKALI na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wametakiwa kukaa chini kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ili kuepusha vurugu kutokea nchini maandamano hayo yatakapofanyika.
Rai hiyo ilitolewa na Taasisi ya Maridhiano inayoundwa na viongozi mbalimbali wa dini jijini Dar es Salaam jana.
Lengo la taasisi hiyo ni kuishauri serikali na kutafuta suluhu na viongozi wa Chadema walioanzisha operesheni hiyo.
Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Mchungaji Osward Mlay, alisema ili kuepuka machafuko yanayoweza kutokea wakati wa kutekeleza operesheni hiyo Septemba mosi, mwaka huu huku Jeshi la Polisi likisema litauvunja Ukuta ni vyema pande zote mbili zikajadiliana na kupata mwafaka.
"Hakuna jambo lililoshindikana mezani. Sisi kama taasisi ya maridhiano, tunaiomba serikali ikae mezani na viongozi wa Chadema ili kumaliza tofauti," alisema.
Mchungaji Mlay aliongeza kuwa sababu ya kuwashawishi Chadema na serikali kufanya maridhiano ni kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha amani ya nchi inadumu na kuondokana na dhana ya viongozi wa dini kutafuta usuluhishi pindi machafuko yanapotokea.
Alisema wana jukumu la kuwashauri viongozi wote wa serikali pale wanapohisi kunaweza kutokea uvunjifu wa amani na kwamba hawako tayari kukaa kimya pindi wanapoona ishara ya vitendo hivyo kama lilivyo lengo lao.
Mchungaji Mlay pia aliitaka Chadema kusitisha maandamano waliyopanga kufanya na badala yake wakae mezani kuona namna wanavyoweza kudai demokrasia kwa amani badala kutumia njia ya maandamano.
Pia alivishauri vyombo vya dola kuongoza nchi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamiwa na Katiba ya nchi bila kukandamiza demokrasia.
Alisema wananchi pia wanapaswa kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani kama kufanya maandamano yasiyo na tija kwa taifa ili kusitokee vurugu zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Naye Sheikh Mohamed Hariri, alisema wanategemea serikali na Chadema watatafuta suluhu badala ya kusubiri machafuko yatokee.
Blogger Comment