Baada ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kumsimamisha uanachama yeye na wanachama wengine 10, 28 Agosti mwaka huu, jumuiya mbalimbali za chama hicho ikiwemo ile ya wazee na ile ya vijana (JUVICUF), zote kwa nyakati tofauti zilijitokeza kubariki uamuzi huo.
Leo asubuhi, jumuiya ya vyuo vikuu ya Chama cha Wananchi – CUF, tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imejitokeza na kukemea vikali matendo ya sasa ya Prof. Lipumba na kusisitiza kuwa yanalenga kukivuruga chama.
“Tunalaani fujo na kauli za kibaguzi zinazoendelea kutolewa na aliyekuwa mwenyekiti wa CUF taifa pamoja na wafuasi wake, wakijaribu kupinga maamuzi halali ya chama ya kukubali kujiuzulu kwake,” amesema Chande Jidawi, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo
Chande amesema, ni wazi kuwa Prof. Lipumba hana nia njema na CUF, bali ana nia ya kukigawa chama hicho, jambo linalopaswa kupingwa na kukemewa na kila mwanachama wa chama hicho anayekitakia mema chama.
Itakumbukwa kuwa, mkutano mkuu wa CUF taifa, uliidhinisha uamuzi wa Prof. Lipumba kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, 21 Agosti katika ukumbi wa hoteli ya Blue Peal, jijini Dar es Salaam hata hivyo, wanaosadikiwa kuwa wafuasi wake walizua vurugu na kusababisha kuahirishwa kwa mkutano huo.
Ni baada ya kuahirishwa kwa mkutano mkuu huo, ndipo 28 Agosti mwaka huu, baraza kuu la uongozi la chama hicho lilifikia uamuzi wa kumsimamisha uanachama Prof. Lipumba na wanachama wengine 10, wakiwemo wabunge na maofisa wa makao makuu ya CUF taifa.
Tangu kutangazwa kwa uamuzi huo, Prof. Lipumba amekuwa akijinasibu katika vyombo vya habari mbalimbali kuwa, yeye bado ni mwenyekiti halali wa chama hicho. Ingawa hajawahi kunukuliwa akieleza kipengele chochote cha katiba ya chama hicho inayompa uhalali kuendelea kuwa mwenyekiti.
Akieleza kile alichokiita ushauri wa bure kwa Prof. Lipumba, Chande amesema, “Tunamshauri aachane mara moja na mpango wake wa kuvuruga chama kwani kwa sasa, anajidhalilisha na kujishushia heshima aliyojijengea miaka mingi katika jamii ndani na nje ya nchi.
Si tu anajidhalilisha yeye pekee bali pia anaidhalilisha jamii ya wasomi wenye hadhi kama yake.”
Amefafanua zaidi kuwa, Prof. Lipumba alikuwa mwenyekiti wa CUF kwa mujibu wa Katiba ya CUF toleo la mwaka 1992 iliyofanyiwa marekebisho ibara ya 91(1), na alitumia ibara 117(1) inayompa uhuru kiongozi yoyote kujiudhulu wadhifa wake.
“Ibara ya 117(2) inaelekeza kiongozi yoyote atakayejiuzulu, lazima barua yake ipelekwe kwenye mamlaka iliyomteua au kumchagua ili kufanyia uamuzi barua hiyo ya kujiuzulu. Hivi ndivyo ilivyokuwa katika mkutano mkuu uliofanyika mwezi uliopita, mkutano mkuu ulikubali kujiuzulu kwake,” amesisitiza Chande.
Blogger Comment