ARUSHA: Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wimbi la miili ya marehemu kuchanganyiwa ndugu linazidi kutikisa nchi baada ya mwili wa mtoto Brian Kamnde (1/6) uliokuwa umezikwa kwa saa 24, kulazimika kufukuliwa kufuatia kubainika kuwa, siyo uliyokusudiwa na kwamba, ulikuwa ni wa mtoto Valentino Alfa Makundi (0/4), Uwazi lina kisa kamili.
ENEO LA TUKIO
Tukio la kufukuliwa kwa mwili huo, lilijiri Mtaa wa Lorovono, Kata ya Sokoni jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kubainika kuwa, mwili huo ulitolewa kimakosa katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti (mochwari) kwenye Hospitali ya Mkoa, Mount Meru.
Mkanganyiko wa tukio hilo ulitokana na ndugu wa marehemu Brian aliyefukuliwa Mtaa wa Lorovono kufika mochwari kwa lengo la kumchukua mpendwa wao huyo na kupigwa butwaa baada ya kutafutwa kwa marehemu huyo bila mafanikio.
MAELEZO YA MAMA MZAZI
Mama mzazi wa Brian, Neserian Elisha, mkazi wa Nambere jijini hapa, alisema kuwa baada ya kufika mochwari kuchukuwa mwili wa mtoto wake hawakuuona na kuoneshwa mwili wa Valentino.
SITOFAHAMU YAIBUKA
Hali hiyo ilizua sintofahamu kwa upande wa wanandugu hao, ndipo uongozi wa mochwari hiyo walipolazimika kufuatilia na kubaini kwamba, mwili wa Brian ulitolewa kimakosa na kuwataka ndugu waliouzika eneo la Sokoni kufika mochwari hapo haraka ili kuutambua mwili wao sahihi. Wakati huo tayari mwili wa Brian ulikuwa umeshazikwa jana yake.
LAWAMA ZA MHUDUMU WA MOCHWARI
Francis Coster ni mmoja wa wahudumu wa chumba cha maiti, yeye alisema tukio hilo lilisababishwa na wanandugu kutokuwa makini wakati wa kuchukua mwili wa marehemu wao.
BABA MDOGO WA MAREHEMU
Kwa upande wake, baba mdogo wa marehemu, Valentino, Godson Makundi alisema wamesikitishwa sana na tukio hilo na kuongeza kuwa ni la aibu kwa hospitali.
“Sisi baada ya kufika katika chumba cha maiti tulikuta umati wa wananchi ambao walikwenda kuchukua miili ya ndugu zao waliopata ajali iliyotokea hapa Arusha, hivyo hatukuruhusiwa kuingia, bali walitutaka kuonesha karatasi yenye utambuzi wa marehemu na kutolewa akiwa ameshaoshwa na kusitiriwa kwenye jeneza. Tukaenda kuzika, kesho yake tukashangaa kuambiwa tulizika mwili ambao haukuwa wa mwanetu,” alisema Makundi.
MAMA MZAZI AZIMIA
Wakati wa kulifukua jeneza lenye mwili wa Brian ambapo usahihi lilitakuwa kuwa na mwili wa Valentino, mama wa Valentino alipoteza fahamu baada ya kujiridhisha kuwa, mwili huo haukuwa wa mwanaye.
MIILI YAENDA KUZIKWA
Mwili wa marehemu Brian ulipelekwa kuzikwa tena eneo la Mbokomu wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro huku mwili wa Valentino ukienda kuzikwa kwenye kaburi lilelile lilofukuliwa Mtaa wa Lorovono.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa tukio na kusema wao ndiyo waliotoa kibali cha kufukuliwa kwa mwili huo ili ukazikwe eneo lililostahili.
GUMZO KUBWA, MUHIMBILI YATAJWA
Tukio hilo limezua gumzo kubwa na kuacha waombolezaji vinywa wazi ambapo baadhi ya wananchi wa Jiji la Arusha wamesema ni la aibu na la aina yake huku wengine wakikumbushia matukio mawili ya miili kubadilishwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar.
Hospitali ya Taifa Muhimbili iliwahi kuingia kwenye mkasa kama wa Arusha mara mbili baada ya Aprili mwaka huu, kutoa mwili wa marehemu kwa watu tofauti ambao nao bila ya kujua, waliusafirisha na kuuzika Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa Janeth Bambalawe (65) wa Gongo la Mboto uliozikwa Usangi ulirejeshwa Dar ili ukabidhiwe kwa wahusika ambapo ulichanganywa na mwili wa Amina Msangi (79) uliostahili kuzikwa Usangi.
Pia, Juni mwaka huu, Muhimbili ilirudia kosa hilo kwa kuruhusu mwili wa marehemu kuchukuliwa na ndugu wasiohusika na hivyo kuleta mtafaruku mkubwa ambapo mwili wa mwanafunzi aliyekuwa kidato cha tatu, Shule ya Sekondari Ulongoni, Dar, Mamy Venancy ulienda kuzikwa Mtwara kwa kuuchanganya na wa marehemu aliyetajwa kwa jina moja la Theresia, mwenyeji wa Mtwara.
Blogger Comment