Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe ameagiza wenyeviti wa halmashauri 18 nchini
zinazoongozwa na Ukawa kuacha utaratibu wa kutoa fedha za halmashauri
kuwasaidia mafuta ya magari wakuu wa wilaya au kuzitumia kwa ajili ya
masuala ya kisiasa ya vyama vyao.
Akizungumza na mameya na wenyeviti wa halmashauri zinazoongozwa na Ukawa
katika mkutano uliofanyika juzi mjini Arusha, Mbowe alisema viongozi
hao wanapaswa kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa na halmashauri hizo
zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Alisema katika kikao hicho cha mameya na wenyeviti wa halmashauri,
wametambua kuwa kuna matumizi mabaya ndani ya Serikali, mbali na
wafanyakazi hewa ambao wapinzani wamekuwa wakilalamika tangu mwaka 2005.
Mbowe alisema bado kuna halmashauri ambazo zimekuwa zikitumia fedha
kufadhili ofisi za wakuu wa wilaya na chama tawala, jambo ambalo sasa
kwa halmashauri za Ukawa halitakuwapo.
“Maeneo ambayo wakuu wa wilaya wamezoea kuomba fedha za mafuta na CCM
wamekuwa wakiomba fedha kwa ajili ya kazi zao tunawaambia wasithubutu
tena kwenda kwenye halmashauri zinazoongozwa na Ukawa, kwani hatutawapa
fedha na tunawaumbua,” alisema.
Mbowe alisema katika halmashauri za Ukawa hawataki kusikia kuna fedha
zimetolewa kwa wakuu wa wilaya au chama chochote cha siasa.
Alisema katika kikao hicho wamekubaliana kuanzisha mipango mikakati
ambayo itawezesha kubuniwa vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni rafiki kwa
wananchi, kupatikana kwa ajira na kuboresha huduma muhimu za
Watanzania.
Akizungumza baada ya maelekezo hayo, Mwenyekiti wa Madiwani Chadema
nchini ambaye pia ni Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema
watatekeleza na hawatakubali kuingiliwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa
mikoa na makatibu tawala.
Calist alisema katika halmashauri za Ukawa uamuzi wa mwisho wa
uendeshaji wa halmashauri utafanywa na madiwani na siyo mtu kutoka nje
ya halmashauri hizo.
“Tutasimama na kutetea mamlaka ya kisheria ya Serikali za mitaa hapa nchini,” alisema.
Katibu wa Madiwani wa Ukawa nchi nzima ambaye ni Meya wa Kinondoni,
Boniface Jacob alisema watahakikisha wanasimamia utendaji mzuri wa
halmashauri zote wanazoziongoza ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma
bora.
Blogger Comment