Serikali haikukurupuka Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye utalii

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, amewataka Watanzania na wadau wa sekta ya utalii kutambua kuwa serikali haikukurupuka kupeleka pendekezo la kuweka Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye shughuli za utalii, huku akiwataka waelewe kuwa si shughuli zote zilizowekewa ongezeko hilo.
Amesema katika pendekezo hilo lililopitishwa na Bunge, Serikali imezingatia hatua zote ikiwemo kufanya mazungumzo na wadau wa sekta hiyo.
Dk Tizeba ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la kuhudumia mizigo inayoingia nchini la Kampuni ya Swissport.
Ujenzi wa jengo hilo lililojengwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), umegharimu Sh bilioni 30.
Amesema, Sheria ya bajeti ni shirikishi, hivyo kabla ya pendekezo la kuweka VAT kwenye shughuli za utalii, jambo hilo lilipitia hatua mbalimbali, ikiwemo kuwashirikisha wadau wa sekta hiyo, ambao walikubaliana na jambo hilo na hatimaye kupitishwa na Bunge.
"Ieleweke si shughuli zote za utalii zimewekewa kodi ni baadhi tu. Hili jambo lisipotoshwe na kupeleka alama mbaya kwa wadau wetu, kwa sababu neno moja linaweza likaharibu maana nzima," amesema Dk Tizeba.
Ametaka wadau mbalimbali kujua kuwa utalii wa Tanzania haufanani na wa nchi zingine, lakini pia wa nchi hizo haufanani na wa nchini.
Akizungumzia jengo hilo, Dk Tizeba alisema litaongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa zinazoharibika na kuongeza wingi wa bidhaa za ndani kusafirishwa nje ya nchi kwa sababu la awali lilikuwa dogo.
Dk Tizeba aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema ujenzi wa jengo hilo ni mfano mzuri wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP), kwani baadaye jengo hilo litabaki kuwa mali ya umma.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania, Gaudence Temu, alisema teknolojia itakayotumika kwenye ghala hilo italifanya kuwa la kipekee barani Afrika.
Amesema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ilitwaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo chini ya Jenga, Tumia na Hamisha (BOT) kwa makubaliano ya jengo na ardhi kubaki kwa mamlaka hiyo baada ya miaka 15, baada ya kusaini mikataba ya umilikishwaji.
Kwa mujibu wa Temu, jengo hilo jipya litakuwa ni kwa ajili ya kuhudumia mizigo inayoingia nchini na jengo la zamani kwa sasa litakuwa ni la kuhudumia mizigo inayoenda nje ya nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment