MOJA YA NJIA ZA KUKUFANYA UFURAHIE MAPENZI

Image result for african brides at 50
KILA mmoja anahitaji kufurahi katika mahusiano yake. Hakuna asiyependa hali hiyo. Mapenzi ni raha, furaha na ni suala la amani ya nafsi, sasa kwanini mtu achukie?
Ila mbali na ukweli huo, ni watu wachache sana wanaofurahia mahusiano yao ya kimapenzi, ukiachana na zile siku za mwanzo za upya wa penzi lao.
Zile siku ambazo kiujumla ni lazima tu wahusika wafurahie kutokana na upya na ugeni wa kila mmoja kwa mwenzake.
Nyakati zile, watu hufurahia sana uhusiano wao kwa sababu kila mmoja hamjui mwenzake namna inavyopaswa. Katika nyakati hizi, watu hujuana zaidi katika upande wa ubora wao, si udhaifu wao. Hivyo watu hudanganyika zaidi na ule ubora na kuamini maisha yako hivyo na yatakuwa hivyo daima.
Watu wengi baada ya kupitisha miezi kadhaa katika mahusiano yao huanza kujikuta katika hali ya tofauti kiasi. Hali ya kutofurahia kwa ukamili mahusiano yao kama ilivyokuwa mwanzo. Katika hili kuna sababu nyingi. Ila leo tutakwenda kuiona moja tu.
Wapenzi wengi hujikuta wakipoteza raha na amani katika mahusiano yao kutokana na kupenda kuchukulia kila tendo au neno la mwenzake katika uzito wa juu. Hapo bila kuangalia mhusika aliongea au alitenda jambo hilo katika hali gani. Kama ni ya utani, alidhamiria au bila kujua. Wao hilo hapana.
Kutokana na kuchukulia mambo katika mtindo huo bila kuangalia wahusika wametenda kwa namna gani au kwa sababu gani, wengi wa wapenzi wamejikuta wakipoteza morali na ile hali ya furaha waliyokuwa nayo kwa wapenzi wao.
Ni vyema ikaeleweka kuwa kila binadamu ana tabia ambayo inampa utofauti na mtu mwingine. Unaweza kuwa umefanana na fulani karibu kwa kila kitu, ila kuna kitu ambacho ni lazima tu utakuwa umetofautiana naye. Hiyo haijalishi ni katika mazungumzo au matendo. Sasa hapa ndiyo kunaleta shida kidogo.
Wengi baada ya kuwa na kina fulani katika mahusiano yao wanapenda wafanane nao karibu kwa kila kitu ili aweze kujiridhisha katika nafsi yake kuwa aliye naye ndiyo chaguo lake kamili. Kitu ambacho hakiwezekani.
Unakuta anaanza kumfuatilia kwa kina na kutoa tafsiri kuanzia katika maongezi yake mpaka matendo yake. Ukiwa hivi kwa mwenzako ni lazima tu utampata na kasoro. Na hizi kasoro kimsingi ukiendelea kuzitafakari katika mrengo wa kuhukumu ni lazima tu katika mapenzi yenu kuanze kujitokeza dosari.
Ndiyo, ni vyema tukawajua wapenzi wetu ili kuwa na amani na kuwa na uwezo wa kuwapa raha na faraja pia. Lakini siyo katika mtindo huu.
Kitu au binadamu yeyote ukianza kuwa na mashaka naye ni lazima tu utaona matendo yatakayokufanya uhisi unaibiwa, unadharaulika au ana mtazamo tofauti katika mapenzi yenu tofauti na ulio nao.
Na zao kuu la fikra za namna hii ni kumfuatilia sana mpenzi wako kana kwamba umeombwa utoe orodha ya matendo na maneno yake mahala. Katika aina hii ya maisha huwezi kufurahia mapenzi.
Kila mtu kwako atakuwa hafai. Maana katika ufuatiliaji wako wa namna hiyo katu huwezi kumkuta bila kitu cha kukufanya upatwe mashaka. Na hiyo si kwa mpenzi au mke wako tu.
Ni kwa kila mtu ukifanya hivyo basi utakuta kuna vitu vya kukupa mashaka katika maisha yako. Ebu kuanzia leo anza kuwa na wasi wasi na rafiki zako wanaokuja nyumbani kwako.
Tengeneza picha mmoja wao anakuchukulia dada yako au mkeo kisha anza kuchunguza kwa kina kabisa. Ni lazima tu utapata viunganishi vya kumtia hatiani hata kama siyo.
Wasiwasi ukiuendekeza huleta picha kamili hata kama si halisi. Jiamini kwa mpenzi wako. Si ulimtongoza na akakukubali bila kumshurutisha? Sasa hofu ya nini. Anakupenda tu huyo, kama hakupendi si angekuambia?
Au huamini matendo yako kwake kama yanamfurahisha? Sasa dawa si kuwa na wasiwasi, badala yake ni kumfanyia mwenzako vitendo vya kumpa raha na furaha. Wasiwasi wako siyo dawa wala kinga, ni mabadiliko yako tu ndiyo yatakayomfurahisha.
Badala ya kupoteza muda kwa kuwa na wasiwasi, jiimarishe kimatendo na kimaneno kwa mwenzako ili azidi kuvutiwa na kusisimkwa kwa sababu yako. Wasiwasi zaidi ya kukutesa na kukunyima fursa ya kufurahia mapenzi, hauna msaada mwingine kwako.
Kuwa bora kadri unavyoweza, huku ukiamini mahali ulipo ni salama, mfanye mwenzako ajihisi bahati kuwa na wewe. Jitoe kwa mwenzako bila kusita ili afurahie mahusiano na wewe, kama akiacha kufurahia mahusiano na wewe basi hata yeye hawezi kufanya jambo la kukufurahisha. Kwa leo tuishie hapa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment