TATIZO la kuketi kwa muda mrefu ni mojawapo ya matatizo yanayoongezeka kwa kasi hapa nchini.
Mabadiliko ya kiuchumi kwa kiasi kikubwa yamechangia kusababisha tatizo hili. Mpaka hapa wengi wenu mnaweza mkawa mnajiuliza–ni nini haswa sababu ya kusema kuketi kwa muda mrefu ni tatizo, wakati wengi wetu tukidhani ni starehe.
Kuketi kwa muda unaozidi saa nane kwa siku kunaweza kukusababisha kifo, ambacho katika hali ya kawaida kinazuilika. Utafiti mkubwa uliofanyika kwa zaidi ya miaka 12 huko nchini Marekani umebainisha hayo.
Katika utafiti huu wataalamu waliwafuatilia wanawake takribani 100,000; kwa muda wa miaka isiyopungua 12. Utafiti huu ambao ulianza mwaka 1993 ulihusisha wanawake wenye umri kati ya miaka 50-79, na uliendelea mpaka mwaka 2010.
Wanawake hawa walirekodi muda waliokuwa wakiutumia kuketi, na watafiti waliendelea kuwafuatilia wanawake hao mara kwa mara.
Kutokana na muda waliokuwa wakiutumia kuketi, wanawake hawa waligawanywa katika makundi manne.
Wale waliokuwa wakitumia chini ya saa nne kuketi, waliokuwa wakitumia kati ya saa nne mpaka nane kuketi, walikuwa wakiketi kwa muda wa saa kati ya nane na 11, kundi la mwisho ilikuwa ni wale waliotumia zaidi ya saa 11 kwa siku, wakiwa wameketi.
Baada ya kuwafuatilia wanawake hawa kwa takribani miaka 12, ilionekana kwamba, ukilinganisha na wale waliotumia saa chache kuketi, asilimia kubwa ya wanawake waliotumia muda mwingi zaidi kuketi walipoteza maisha katika kipindi hicho cha miaka 12.
Vifo hivyo vilivyowakuta wanawake hawa vilitokana na sababu tofauti tofauti vingi vikiwa vinatokana na mojawapo ya magonjwa sugu kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na aina fulani ya saratani.
Cha kustaajabisha zaidi ni ukweli kwamba, namba ya waliopoteza maisha katika wale waliokuwa wakitumia zaidi ya saa 11 kuketi, ilikuwa kubwa kuzidi wale waliokuwa wakitumia kati ya saa nane na 11.
Namba ya waliopoteza maisha katika hawa waliokuwa wakitumia kati ya saa 8-11 kuketi ilikuwa kubwa kuliko ile ya wale waliokuwa wakiketi kwa saa 4-8.
Na kiasi kidogo mno cha wale waliokuwa wakitumia chini ya saa nne kuketi, walipoteza maisha. Hii inaonyesha kwamba kadri muda au dosi ya kuketi inavyoongezeka, hivyo hivyo hatari ya kupoteza maisha kutokana na magonjwa sugu inaongezeka.
Utafiti huu ni mmoja kati ya tafiti nyingi zilizofanyika sehemu mbalimbali za dunia, na kuonyesha kwamba kuketi kwa muda mrefu kunatuongezea uwezekano wa kupata magonjwa sugu hivyo kukuweka katika hatari ya kufikwa na mauti inayoweza kusababishwa na magonjwa hayo. Kuketi kwa muda mrefu kunachangia kwa kiasi kikubwa kusababisha maumivu sugu ya mgongo na hata magoti.
Upo ushahidi wa kiutafiti unaoonyesha watu kupata ulemavu wa kudumu kwa ajili ya kuketi kwa muda mrefu.
Kuna tafiti zilizoonyesha kwamba mtu mmoja kati ya watu wawili wanaotumia kompyuta mara kwa mara ana matatizo sugu ya misuli na viungo yanayotokana na kuketi kwa muda mrefu.
Ziko hata tafiti zinazoonyesha kwamba, hata kama unatimiza kiwango cha mazoezi kinachoshauriwa katika kujikinga na magonjwa, kutumia zaidi ya saa nane ndani ya siku moja kuketi ni hatari.
Ikumbukwe kwamba, tunapozungumzia kuketi kwa saa nane, haimaanishi kuketi kwa saa nane mfululizo, bali ukijumlisha saa zote unazokuwa umeketi hususani katika saa 12 ya mchana, muda huo ufike saa nane au zaidi.
Kwa kawaida tunaketi tukiwa katika magari, maofisini, na tunapokuwa nyumbani tukiangalia TV.
Wanasayansi bado wanafanya tafiti ili kulifahamu kwa undani tatizo hili. Hata hivyo, ni vizuri kufahamu kwamba kuketi kwa muda mrefu, hususan zaidi ya saa nane kwa siku, kiafya si kitu kizuri.
Kama wewe ni mmoja ya watu ambao shughuli zao za kila siku zinawalazimu kuketi kwa muda mrefu, unaweza kabisa ukawa unajiuliza unafanya nini kuepukana na tatizo hili.
Hizi hapa njia mbili
zilizofanyiwa tafiti na kuhakikiwa katika kupunguza athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na kuketi muda mrefu:
Mapumziko mafupi ya mara kwa mara
Kwa mtu mwenye kazi inayomlazimu kuketi muda mrefu, tafiti zimeonyesha kwamba kupumzika na kusimama au kutembea angalau kila baada ya saa moja kunasaidia kupunguza makali ya athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na kuketi kwa muda mrefu.
Jiwekee mapumziko ya takribani dakika tano mpaka 15, ambako unautumia muda huo kusimama, kutembea au kujinyoosha.
Kubadilisha mkao wa mwili (posture) kila baada ya dakika 30
Hii kitaalamu inaitwa seat-stand posture yaani kukaa na kusimama. Maana ya hii ni kwamba kazi inakuwa inaendelea kama kawaida ila unaweza kufanya ukiwa umekaa au umesimama.
Unaweza kuketi wakati unachapa kwenye komputa yako na kuamua kusimama wakati unapangilia vitu vyako mezani. Tayari kuna meza na viti maalumu kwa ajili ya zoezi hili na zipo kampuni ambazo zimeshaanza kutumia vifaa hivi.
Ziko njia nyingine nyingi za kupunguza athari za kuketi muda mrefu kwa afya zetu.
Mwandishi wa makala hii ni Daktari bingwa wa fisiolojia ya homoni na mazoezi. Kupata ufahamu zaidi kuhusu mazoezi, mitindo ya maisha na afya tembelea youtube channel ya daktari hewani.
Blogger Comment