WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema kuwa serikali imepiga marufuku biashara ya kusafirisha wanyama hai nje ya nchi mpaka pale itakapowekwa misingi mizuri kuwezesha nchi kunufaika na biashara hiyo.
Profesa Maghembe ameyasema hayo wakati wa kipindi cha "Tunatekeleza" kinachoandaliwa na Idara ya Habari-Maelezo kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Amesema, serikali iliamua kuangalia upya utaratibu huo wa kuuza wanyama hai na kuamua kusitisha biashara hiyo hadi pale utaratibu na misingi mizuri ya biashara hiyo itakapowekwa.
“Ni kweli kulikuwa na utaratibu wa kuuza wanyama hai nje ya nchi bila kuiwezesha nchi kupata faida yoyote ile, hivyo kwa sasa kama nchi tumeamua kupiga marufuku biashara hiyo kwa maslahi ya taifa.
“Haiwezekani uuze wanyama hai nje, halafu anayenufaika ni yule anayenunua na kuiacha nchi bila faida yoyote ya uwepo wa maliasili hiyo, hivyo kama nchi tumeamua kupiga marufuku biashara hiyo hadi pale misingi mizuri ya kibiashara itakapowekwa na kuiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake,” amesema Maghembe.
Aidha, Profesa Maghembe amesema, kwa sasa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ujangili wa wanyamapori kama tembo na faru ikiwemo kukamata watu wote wanaohusika katika biashara hiyo na mpaka sasa wameshakamata baadhi ya watu akiwamo mwanamama anayejiita malkia wa pembe za ndovu ambaye anadaiwa kuwa kinara katika biashara hiyo.
Akizungumzia wizi katika mazao ya misitu, Profesa Maghembe amesema, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kupambana na wizi wa mazao ya misitu na imekubaliwa kuwa iwapo gari litakamatwa likiwa na mazao hayo bila kuwa na kibali, Serikali itataifisha gari hilo na wahusika watashtakiwa kama wahujumu uchumi.
Amesema, serikali imeahidi kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki kwenye vijiji vilivyo pembezoni mwa misitu ili kuweza kudhibiti uchomaji moto kwenye kwenye maeneo hayo, hali itakayowezesha pia utunzaji wa mazingira.
Blogger Comment