Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kufuatia mvutano wa kusimamishwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Profesa Lipumba kumuandikia barua Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akilalamikia kusimamishwa uanachama bila kufuata utaratibu huku akitaka kurejeshwa kwenye nafasi yake ya uenyekiti.
Ofisi hiyo imeutaka uongozi wa CUF kueleza kwa kina hatua ilizopitia hadi kufikia uamuzi huo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, na kwamba iwasilishe barua hiyo kufikia kesho majira ya saa 9:30 alasiri.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano cha Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Monica Laurent amesema kuwa ofisi hiyo ilipokea barua ya Profesa Lipumba Agosti 29 mwaka huu ikiwa na malalamiko na kwamba wametaka uongozi wa CUF kutolea majibu.
“Tumeitaka CUF kutoa majibu kuhusu malalamiko ya Profesa Lipumba, ndipo sisi tutakapotoa majibu,” amesema Monica.
Lipumba ambaye alijiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti mwaka jana akipinga uamuzi wa chama chake kumuunga mkono Edward Lowassa kugombea urais, amerejea na kudai kutengua barua yake ya kujiuzulu.
Baraza Kuu la CUF lililoketi visiwani Zanzibar hivi karibuni lilimsimamisha uanachama Profesa Lipumba pamoja na viongozi wengine 10 akiwemo Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu Katibu mkuu (Bara).
Hata hivyo, Profesa Lipumba amepinga uamuzi huo akieleza kuwa kikao cha baraza hilo kililiwa batili.
Blogger Comment