Makamu wa Rais atoa onyo kwa wanaosafirisha Korosho kwa Magendo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemaliza ziara yake ya siku NNE mkoani Mtwara kwa kuwahakikishia mamia ya wakazi wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kuwa serikali imetenga zaidi ya bilioni 170 kwa ajili ya utekeleza wa mradi mkubwa wa maji katika wilaya hiyo ili kuondoa tatizo la uhaba wa maji kwa  wananchi wa Tandahimba.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tandahimba na wakati amesimamishwa njiani na wananchi wa vijiji vya Kitama I na Kitama II  ambao walitaka kumsalimia akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.

Makamu wa Rais amesema mkakati wa serikali wa sasa unalenga kuhakikisha wananchi wa Tandahimba na wa maeneo mengine nchini wanapata maji safi na salama hali ambayo itaondoa usumbufu wa wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Amesema anaimani kubwa kuwa mradi huo wa maji utakapokamilika wilayani Tandahimba mkoani Mtwara utakuwa ni suluhu ya kudumu ya uhaba wa maji kwa wananchi hao wa Tandahimba.

Kuhusu usafirishaji wa korosho kwa njia ya magendo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameonya kuwa serikali kamwe haiwezi kuwavumilia watu wanaofanya vitendo hivyo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

Makamu wa Rais amesema kuwa biashara ya magendo ya korosho inainyima serikali mapato mengi ambayo yangesaidia shughuli za maendeleo za wananchi hivyo ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mtwara uchukue hatua za kukomesha biashara hiyo haramu ambavyo ameifananisha na uhujumu uchumi kwa serikali.

Kuhusu ubovu wa barabara kutoka mjini Mtwara hadi wilaya ya Tandahimba, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali itajenga kilomita 50 za awali kwa kiwango cha lami katika barabara hiyo ili kuimarisha shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya Mtwara mjini na wilaya ya Tandahimba.

Makamu wa Rais pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mtwara kukutana haraka na Watendaji wa Wakala wa Barabara wa mkoa wa Mtwara ili kujadiliana kuhusu namna gani ujenzi huo utakavyotekelezwa.

Akiwa mjini Tandahimba, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika zoezi la utoaji wa zawadi mbalimbali kwa uongozi wa shule ya sekondari ya Tandahimba kwa kuingia katika shule 10 bora kitaifa katika matokeo ya Kidato cha  Sita ambapo Kampuni ya Startimes imetoa hundi ya shilingi milioni Mbili kwajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wilayani humo.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Mtwara.

10-Sep-2016
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment