Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi wananchi wa Kisiwa cha Pemba kutokubali kurubuniwa na watu wanaowachochea kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwa vitendo hivyo vinarudisha nyuma juhudi za kuwaletea maendeleo na kutatua kero zinazowakabili.
Rais Magufuli amesema hayo tarehe 02 Septemba, 2016 wakati akihutubia Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Gombani ya Kale Wilaya ya Chakechake Mkoani Kusini Pemba, ambao umehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.
Rais Magufuli amesema Kisiwa cha Pemba kina fursa nyingi za maendeleo ikiwemo Uvuvi wa baharini, Utalii na Kilimo lakini endapo wananchi wataendelea kushabikia uchochezi na vitendo vya kuvuruga amani vinavyofanywa na baadhi ya watu, hakuna mwekezaji atakayekuwa tayari kuwekeza.
""Hawezi akaja mtu kujenga kiwanda wakati hakuna amani, sisi vijana lazima tuwe mstari wa mbele kujenga amani ili wawekezaji waje wajenge viwanda na tupate ajira.
"Hapa Pemba kuna fukwe nzuri ambazo zinafaa kujenga hoteli kubwa za kitalii, nani atakuja kujenga hoteli kama hakuna amani?" Amehoji Rais Magufuli huku akisisitiza kuwa umefika wakati kwa wananchi wa Pemba kubadilika na kujikita katika masuala ya maendeleo.
Hata hivyo Rais Magufuli ameonya kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitawafumbia macho watu wanaofanya uchochezi unaolenga kuvuruga amani na ameviagiza vyombo vya dola vianze kuwafuatilia wote walioanza kufanya uchochezi huo.
Amesisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki sasa ni kwa watanzania kufanya kazi na kujenga nchi yao.
Mapema akimkaribisha Rais Magufuli kuzungumza na wananchi hao, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amewaambia wananchi wa Zanzibar kuwa tangu aingie madarakani yeye na Rais Magufuli wamefanya mambo mengi kwa manufaa ya Watanzania
Dkt. Shein ameongeza kuwa hali ya Muungano ni nzuri na kwamba sehemu kubwa ya kero za Muungano zimetatuliwa huku akibainisha kuwa kwa sasa kazi iliyopo ni kutafuta changamoto mpya za Muungano zenye lengo la kuchochea maendeleo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mke wa Rais Magufuli Mama Janeth Magufuli na Mke wa Rais Shein, Mama Mwanamwema Shein, Mawaziri na viongozi mbalimbali wa Siasa, Dini na Serikali.
Jioni hii (jana) Rais Magufuli amewasili mjini Unguja ambapo kesho tarehe 03 Septemba, 2016 ataendelea na ziara yake kwa kuzuru kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Sheikh Abeid Amaan Karume, kuzuru kaburi na kutoa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi na baadaye atazungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti Mjini Unguja.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Unguja
02 Septemba, 2016
Blogger Comment