Waziri Mkuu Ayakataa Madawati Yaliyotolewa Na Tfs


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekataa kupokea msaada wa madawati uliotolewa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) baada ya kubaini yametengenezwa chini ya kiwango.

“Ofisa Elimu njoo kagua haya madawati yaliyo mazuri nitayapokea na yaliyobaki yarudishwe karakana yakatengenezwe upya huu si wakati wa kupokea vitu vibovu,“ amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 02, 2016) wakati alipowasili katika kiwanja cha Mabau, Mtibwa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi ambapo alikabidhiwa madawati hayo na Meneja wa TFS….

Alisema anatambua dhamira ya TFS ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kumaliza tatizo la upungufu wa madawati lakini hawezi kupokea kupokea madawati yaliyotengenezwa chini ya kiwango.

Baada ya Ofisa Elimu (Msingi) wa Wilaya ya Mvomero, Michael Ligola kukagua madawati 102 yaliyoletwa uwanjani hapo madawati 84 yalibainika kuwa ni mabovu na 14 tu ndiyo yalikuwa mazima.

Waziri Mkuu alisema hawezi kupokea madawati hayo yaliyotolewa na Meneja wa Msitu wa Mtibwa, Hamza Kateti na kuuagiza uongozi wa wilaya ufuatilie suala hilo kwa kuwa walitakiwa kuyakagua kabla ya yeye kukabidhiwa.

Katika hatua nyingine aliwasisitiza wazazi na walezi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Serikali imewapunguzia mzigo kwa kuwaondolea michango na ada hivyo tumieni fursa hiyo kwa kuwapeleka shule watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule na wasimamie masomo yao,”alisema.

Awali mbunge wa jimbo la Mvomero, Saddiq Murad alisema miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni pamoja na wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba hivyo amemuomba Waziri Mkuu kuingilia kati suala hilo.

Akizungumzia namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo michache watatengewa maeneo katika vijiji.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment