Ugonjwa wa Sumukuvu Wahatarisha Maisha Nchini........Umeua Watu 14 Mpaka sasa Huku 54 Wakiwa Wanaugua Ugonjwa Huo


Watu 14 wamefariki dunia katika wilaya za Chemba mkoani Dodoma na Kiteto mkoani Manyara kutokana na ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama ‘Aflatoxicosis’ unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka iliyoharibika.

Hayo yamesema na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya magonjwa ya milipuko na magonjwa mengine leo jijini Dar es Salaam.

“Ugonjwa uliosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) uliripotiwa kwa mara ya kwanza tarehe 13 Juni, 2016 katika wilaya za Chemba mkoani Dodoma na baadaye mkoani Manyara katika wilaya ya Kiteteo” alisema Waziri Ummy na kuongeza kuwa:

“Wagonjwa walikuwa na dalili za kuumwa tumbo, kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba na kuwa manjano sehemu mbalimbali za mwili ambayo inaashiria kuathirika kwa ini”

Alisema mbali na vifo hivyo, hadi kufikia Julai 31 mwaka huu wagonjwa 54 waliripotiwa kuugua ugonjwa hu huku wagonjwa wanne wakilazwa kutokana na kuugua.

“Hadi kufikia tarehe 31, July 2016 kulikuwa na wagonjwa 54 na watu 14 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.Aidha katika wiki iliyopita aliripotiwa mgonjwa mmoja mpya kutoka wilaya ya Kondoa”alisema Waziri Ummy na kufafanua kuwa:

“Jumla ya wagonjwa waliolazwa wodini ni wanne kati yao mmoja yupo Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na watatu wapo katika Hospitali ya Kondoa”

Waziri Ummy alitaja wilaya zilizoripoti wagonjwa hao na idadi ya wagonjwa kuwa ni wilaya ya Chemba wagonjwa 38, Kondoa wagonjwa tisa , Kiteto wagonjwa watatu, Chamwino wagonjwa wawili na Dodoma Manispaa  mgonjwa mmoja.

“Vijiji vilivyoathirika zaidi na ugonjwa huo ni kutoka wilaya ya Chemba ambavyo ni Kinkima, Itolwa, Mwailanje na katika wilaya ya Kondoa ni kijijini cha Ubembeni” alisema Waziri Ummy.

Hivyo, aliitoa hofu familia iliyopoteza watu wanne katika kijiji cha Mwaikuzabe na kusema vifo hivyo havihusiani na uchawi au kuwekewa sumu bali ni chakula cha siku ile kilithibitika kwamba kilikuwa na sumukuvu.

Kufuatia athari hizo Serikali itafanya uchunguzi wa kina katika wilaya kumi  za Chemba, Kondoa, Chamwino na Kiteto na wilaya nyingine za mikoa ya Sindida, Dodoma na Manyara zinazopakana na wilaya hizo.

Alisema uchunguzi huo unalenga kubaini hali ya usalama wa vyakula vinavyotumiwa na jamii ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kuwaathiri wananchi wengi zaidi wanaoishi katika wilaya hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taifa wa Afya wa Wizara hiyo Dkt. Fausta Mosha alisema wizara imeandaa  vipepereshi vyenye maelekezo yanayotoa elimu juu ya kijikinga kwa kuandaa chakula kuanzia hatua ya uvunaji shambani hadi wakati wa kula.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Otilia Gowelle alisema njia bora ya kupambana na ugonjwa huo ni kuukinga kwa kuhakikisha sumu kuvu haizalishwi kutoka kwenye nafaka.

Akifafanua kuhusu udhibiti, Waziri Ummy alisema wanashirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi ya uhifadhi na uandaaji wa chakula utakaosaidia kupunguza kiasi cha sumukuvu kwa nafaka ambazo hazijaharibika sana.

“Njia hizi ni pamoja na kuhifadhi nafaka zilizokauka vizuri na kuchambua nafaka zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika rangi” alisema.

Waziri Ummy alisisitiza Serikali kuendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima sumukuvu katika damu na choo kidogo miongoni mwa taasisi za ndani ya nchi.

Inaelezwa kuwa ugojwa wa‘Aflatoxicosis’unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka uliwahi kutokea nchini Kenya mwaka 2004 na kusababisha vifo vya zaida ya watu 100 huku wengine 200 waliathirika.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment