Tundu Lissu Anavyomuelezea Marehemu Jumbe

Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia. Akiwa na miaka 96, Jumbe aliishi muda mrefu sana kwa kigezo chochote kile. Alikuwa mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya January 1964. Alikuwa pia mwasisi wa Muungano ulioizaa Tanzania miezi michache baadae.

Baada ya Sheikh Abedi Amani Karume kuuawa mwezi April 1972, Jumbe aliteuliwa kuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, na alishikilia madaraka hayo hadi January 1984. Wasomi wa Muungano wameandika kwamba wakati Karume anauawa mahusiano yake na Mwalimu Nyerere yalikuwa yameharibika kiasi kwamba Jumbe (kwa upande wa Zanzibar) na Bhoke Munanka (kwa upande wa Tanganyika) ndio walikuwa kiunganishi cha mawasiliano kati ya Mwalimu na Karume. Hii pengine ndio sababu Mwalimu alitumia ushawishi wake kuhakikisha Jumbe anateuliwa kumrithi Karume.

Hata hivyo, Jumbe atakumbukwa zaidi na historia kwa upinzani wake kwa mfumo wa sasa wa Muungano kuliko, pengine, kwa jambo jingine lolote. Jumbe alikuwa mwanasiasa wa kwanza, baada ya era ya Karume, kutambua kwamba muundo wa serikali mbili ulikuwa umeipokonya Zanzibar mamlaka yake na kuyahamishia Tanganyika. Alikuwa wa kwanza kutambua kwamba kuzaliwa kwa CCM, katika context ya Muungano, kulimaanisha mwisho wa mamlaka yaliyokuwa reserved kwa Zanzibar chini ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964.

Sio tu alitambua bali pia Jumbe alichukua hatua kupinga Zanzibar kupokonywa mamlaka yake hayo. Ili kufanikisha azma yake, Jumbe alilazimika kumwachisha kazi Mwanasheria Mkuu wake aliyepewa na Mwalimu Nyerere, Damian Lubuva, na kumwajiri Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy, raia wa Ghana, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kwaw Swanzy ndiye aliyeandaa 'hati ya mashtaka' dhidi ya Muungano iliyokamatwa na watu wa usalama wa Mwalimu na baadae kutumika kumsulubu Jumbe kwenye kikao cha NEC ya CCM Dodoma January 1984.

Kwa sababu ya upinzani huo, Jumbe aling'olewa madarakani pamoja na Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Kwaw Swanzy alitangazwa persona non grata na kufukuzwa nchini. Mwalimu akatangaza 'kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa' Zanzibar na waZanzibari wengi wapinzani wa Muungano, kama Mwanasheria Mkuu wa kwanza Wolfgang Dourado, kuwekwa kizuizini.

Miaka kumi baada ya kuondolewa madarakani, Alhaj Aboud Jumbe alichapisha kitabu chake juu ya Muungano, 'Miaka Thelathini ya Dhoruba', ambako aliweka bayana ugomvi wake na Mwalimu juu ya Muungano. Jumbe ni kiongozi pekee wa juu wa rika la wapigania uhuru wa Tanzania kuandika memoirs zake juu ya Tanzania na matatizo ya Muungano wake. Hata Mwalimu hakufanya hivyo na alikufa na siri zake juu ya mambo mengi makubwa yalitokea wakati wa utawala wake.

Kwangu mimi, hii ndio merit kubwa na mchango mkubwa wa Alhaj Aboud Jumbe kwa kizazi cha sasa na vijavyo vya waTanzania. Alikuwa na ujasiri wa kusema na kuandika juu ya 'The Forbidden Subject', tena katika kipindi cha Mwalimu Nyerere ambapo ujasiri wa aina hiyo ulikuwa ni jambo la hatari kubwa. Kwa sababu hiyo hiyo, Jumbe alilazimika kuishi theluthi ya mwisho ya maisha yake 'kifungoni' Mji Mwema, Kigamboni, ambako alipelekwa mara baada ya kung'olewa madarakani mwaka '84.

Sikuwahi kubahatika kuonana na Alhaj Aboud Jumbe wakati wa uhai wake. Hata hivyo, nimejifunza mengi sana kutoka kwake, hasa ujasiri wa kuuhoji Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jumbe amekuwa na ushawishi mkubwa sana kwenye mjadala wa Muungano kwa zaidi ya miongo mitatu sasa. Ninadiriki kusema kwamba hoja ya Serikali Tatu ilianzia kwa Jumbe.

Roho, spirit, yake ilikuwa kila mahali wakati wa mchakato wa Katiba Mpya kati ya 2011 na 2014. Kivuli chake kilikuwa kila mahali wakati wa Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014. Pengine kuliko hata Mwalimu Nyerere, Jumbe ndiye aliyetufundisha kuufahamu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Atakumbukwa kama mmoja wa waTanzania maarufu na wapigania uhuru wakubwa wa Zanzibar ya baada ya Muungano.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment