Mkuu wa Mkoa aliyetenguliwa, Felix Ntibenda amevunja ukimya na kusema kuwa tuhuma zinazolengwa kwake na Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Mkoa wa Arusha, Philemon Mollel, hazina ukweli wowote.
Alisema kuwa tuhuma za kunyang’anywa Kiwanda cha Usagishaji cha NMC hahusiki nazo na wenye mali ni Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
Mbali na tuhuma hizo Ntibenda alidai kuwa mfanyabiashara huyo alitumia UVCCM kudai kuwa anahusika na uchomaji wa moto katika Shule za Sekondari katika matukio yaliyotokea hivi karibuni.
Alisema UVCCM waliamuru mkuu huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kutoa taarifa kwa umoja huo.
Kauli hiyo aliitoa juzi muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Korona iliyoko nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Alidai kuwa anasikitishwa na kitendo cha Mollel kushirikiana na UVCCM ambao wamekuwa wakieneza propaganda kupitia mitandao ya kijamii kwamba alihusika katika njama za kumnyang’anya kinu hicho.
“Mimi sifanyi kazi kwa amri za chama wala jumuiya bali nafanya kazi na kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa au kwa Rais Dk. John Magufuli na si mtu mwingine wala taasisi nyingine yoyote.
“… nakerwa na tabia ya chama kuingilia shughuli za Serikali kwani maamuzi ya kunyang’anya wawekezaji vinu yalifanywa na Baraza la Mawaziri ambalo lilitaka mali zote zirudi serikalini,” alisema Ntibenda.
Blogger Comment