MWENYEKITI wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustine Mrema ameshauri waathirika wa dawa za kulevya kupelekwa hospitalini kupata tiba badala ya polisi kuwakamata na kuwapeleka mahabusu au gerezani ambapo huko hujazana bila kupata msaada wowote.
Aidha, amesema atamwomba Rais John Magufuli kumrejesha kazini Mwalimu wa Sekondari, Emmanuel Roman ambaye alifukuzwa kwa ajili ya utumiaji wa dawa hizo, lakini hivi sasa ameacha baada ya kupata tiba na ushauri nasaha.
Mrema alitoa ushauri huo jana Dar es Salaam alipokutana na waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya katika Ukumbi wa Friends Corner, Manzese katika Manispaa ya Kinondoni.
Alisema anapopelekwa gerezani mtumiaji wa dawa za kulevya atakuwa hajasaidiwa, kwani atazidi kuharibikiwa badala ya kurekebishwa.
“Ni marufuku kukamata vijana wadogo wanaotumia kete. Sio kama nahamasisha waendelee kutumia ila wakikamatwa wapelekwe hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Temeke ambako kuna vituo vyao. “Ukianzisha operesheni ya kukamata wezi bila kujua historia zao inawezekana ni waathirika wa dawa za kulevya, ambao wanapoanza kutumia kuacha ni kazi sana hivyo wanalazimika kuiba ili wapate hela ya kununua dawa hizo,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa upande mwingine amevitaka vyombo vya usalama kushughulikia wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo maarufu kama `Mapapa wa dawa za kulevya’, badala ya kuhangaika na hao wanaotumia ili kudhibiti hali hiyo.
“Hili nitalifikisha kwa Rais nimwambie taifa lako linaangamia, vijana wanaharibika kutokana na dawa za kulevya, hivyo awashughulikie mapapa wanaoleta dawa kutoka Iran, kwani wanajulikana kwa majina na wengine wanachukua na kusambaza mtaani,” aliongeza.
Alisema kutokana na janga la dawa za kulevya kuzidi kuwa kubwa nchini, atamwomba fedha Rais Magufuli za kuwasaidia waathirika hao kuunda vikundi vya kuzalisha mali.
Pia ameshauri waathirika hao ambao wameacha watumike kukomesha wizi katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwakamata mateja ambao wanawajua.
Blogger Comment