MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Kanindo, Ndalawa Masibuka, ameahidi kuwaongoza wananchi kuwaondoa kwa nguvu wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi, ukaushaji wa masalia ya samaki walioondolewa minofu maarufu kama ‘mapanki’, ifikapo Agosti 30, mwaka huu.
Kwa muda mrefu wananchi wa mitaa ya Kishili na Kanindo wanataka biashara ya ukaushaji ‘mapanki’ kuondolewa kwenye makazi yao baada ya visima vya maji wanayotumia majumbani kuwa na harufu ya samaki.
Mbali na hayo, wananchi hao wanadai kuwa maji hayo pia hubadilika rangi, na kuwa na ladha ya chumvi chumvi, huku miti na mazao mengine yakiendelea kukauka na harufu mbaya ikiendelea kusambaa kwenye makazi yao.
Wakati wananchi wakiweka kusudio hilo, msimamizi mkuu wa wafanyabiashara hao, Rusi Kasubi, akizungumza na MTANZANIA jana, alimtaka Ndalawa asikurupuke kuwaongoza wananchi kwenda eneo hilo Agosti 30, kwani anaweza kujikuta anaingia kwenye migogoro asiyoitarajia.
Alisema anatambua umuhimu wa kuondoa biashara hiyo katika eneo hilo kutokana na uwepo wa makazi ya watu, hivyo anaendelea kutafuta eneo jingine.
Aliongeza kuwa licha ya kupokea barua kutoka kwa afisa afya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kumtaka kuondoa biashara hiyo, ameomba kuvumiliwa.
“Maofisa afya wa kata na jiji walinitembelea Agosti 19 mwaka huu, tena walikuja na Diwani wa Kata ya Kishili, Sospeter Ndumi na huyo huyo Ndalawa anayetaka kunifanyia vurugu, tulizungumza na kufikia mwafaka wa kunipa siku 10 kuhama, sasa kunahitajika maandalizi.
“Kuna maeneo zaidi ya 6 yakiwamo Kanyama-Kisesa, Ihayabuyaga kule Magu, Mkolani na Buhongwa ambayo nafuatilia ili kupata eneo, unapohamia eneo lazima kuwe na maji na barabara ili malori yafike, sasa nimpe onyo Ndalawa na kumtaka asikurupuke maana anaweza kuingia kwenye migogoro,” alisema Kasubi.
Blogger Comment