Lowassa, Mbowe na Katibu Mkuu Chadema Waanza Mikakati ya UKUTA


Siku moja baada ya Chadema kutangaza safu ya Ukuta, viongozi wa chama hicho wameanza kutawanyika mikoani kuanza kutoa elimu ya mpango huo. 

Wakati mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akiwa Kanda ya Kaskazini aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa alikuwa mkoani Mbeya na jana alishiriki ibada na kuanza vikao vya mkakati huo. 

Mbowe jana alikutana na viongozi wa kanda hiyo na kuunda kamati zitakazokwenda katika majimbo yote 35 ya uchaguzi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara kutoa elimu. 

Mbowe alisema katika kikao hicho, ambacho ni mfululizo wa vikao vinavyoendelea kanda zote nchini, wamekubaliana kutoa elimu ya dhana ya Ukuta. 

Hata hivyo, alisema bado chama hicho kimetoa fursa ya mazungumzo kwa taasisi yoyote ili kuhakikisha mgogoro uliosababisha Kamati Kuu kuunda Ukuta. 

Wakati Mbowe akisema hayo, Lowassa ametua katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayojulikana kama Kanda ya Nyasa akiwa na mambo matatu makubwa. 

Aliwasili jana asubuhi kwa ndege ma kwenda moja kwa moja kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Forest akiwa na viongozi wa chama hicho wa kanda pamoja na wabunge mbalimbali wa majimbo ya mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Songwe, Rukwa na wale wa viti maalumu. 

Waziri Mkuu huyo wa zamani, alishiriki ibada ya kawaida na alipokea zawadi ya nyimbo zilizowekwa kwenye ‘flash’ kutoka kwa wanakwaya wa kanisa hilo huku naye akiwachangia kwa kuendesha harambee ya papo kwa papo kutoka kwa viongozi alioongozana nao. 

Katika harambee hiyo, zilipatikana Sh4 milioni zikiwamo Sh 1 milioni ambazo aliahidi kuzitoa. 

Kabla ya ibada kumalizika, Lowassa na ujumbe wake waliondoka kwenda kwenye kikao cha Baraza la Chadema la Kanda. 

Katibu wa Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alitaja mambo matatu makubwa kutoka kwa Lowassa kuwa la kwanza alihimiza wanachama wote kuimarisha umoja na kufuta mipasuko iliyotokea wakati wa uchaguzi. 

Pili, aliwasihi wana Chadema wote kuwa jasiri kwa kupigania haki na kujitambua na la tatu ni kujiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020. 

Mwaisumbe alisema baada ya kikao cha jana, leo Lowassa anaanza kutembelea majimbo ambako atakuwa na vikao vya ndani katika majimbo ya Mbeya Vijijini, Mbozi na Tunduma na kesho atakuwa kwenye majimbo ya Nkasi Kaskazini na Kusini na Sumbawanga wakati kesho kutwa atakuwa Mbarali, Makambako, Njombe Mjini na Mafinga. Agosti 25 atakuwa Iringa Mjini na Kolo. 

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji yupo Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa mitatu; Simiyu, Shinyanga na Mara na jana aliwataka Watanzania kuwapuuza watu wanaodai chama hicho kimejipanga kufanya vurugu Septemba Mosi akisisitiza kuwa maandamano yatakayofanyika ni ya amani. 

Alisema kamwe hawawezi kuvunja sheria na Katiba ya nchi na kwamba kinachofanyika kipo kwa mujibu wa sheria.

 “…Nawaomba Watanzania wote watuunge mkono maana tunachokwenda kukifanya ni kwa ajili ya kuwanusuru watoto wetu wasiingie kwenye matatizo maana kinachoendelea kinakwenda kuondoa demokrasia na utawala bora,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment