CHADEMA Wamwalika Kamanda Sirro Katika Maandamano yao ya UKUTA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Dar es Salaam, kimemkaribisha Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro kujitokeza na kuwa mstari wa mbele kwenye maandamano ya Operesheni Ukuta yatakayofanyika Septemba Mosi.

Kimesema kinamkaribisha kamanda huyo ili kuondoa uwezekano wa kupelekewa taarifa za uongo na askari wake kuhusu maandamano hayo.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam, Benard Mwakyembe, alisema jana kuwa hakuna haja ya kamanda huyo kukaa ofisini bali ajitokeze katika Operesheni Ukuta na awe mstari wa mbele kuwapiga wananchi ambao watatumia muda huo kumuuliza maswala ya sheria kuhusu maandamano hayo.

“Lengo la Operesheni Ukuta ni kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu haifuati sheria bali inafuata mawazo ya mtu mmoja.

“Tumwambie tu kwamba Kamanda Sirro ngoma hii ya Ukuta si ya kitoto, vitisho na mbwembwe zake anazozionyesha barabarani hazitutishi, tupo tayari kwa lolote.

“Tumejiandaa kisaikolojia kwa namna yoyote, tupo tayari kufa kwa ajili ya kuwatetea wananchi, na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, atakuwa mstari wa mbele pamoja na viongozi wengine,”alisema Mwakyembe.

Aidha alisema maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia 99.5 katika mitaa 582 na kata 102 ya jiji zima la Dar es Salaam.

“Niwashukuru Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) kwa kutuunga mkono kuandaa maandamano yao, tunaamini haya ya kwetu yamewapa motisha na kuamua kufanya ya kwao.

“Ninaliomba Jeshi la Polisi liwape ulinzi wa kutosha ingawaje sisi tunajua kwamba huo ni mtego walioufanya kisiasa ili kuleta mabishano ambayo hayana nafasi kwetu,” alisema.

Alisema haki za vyama vya siasa ni kutoa maoni ya kisiasa  kadiri vitakavyoona inafaa, ili kutekeleza sera zake kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment