MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amemmwagia sifa mrembo, Jokate Mwegelo, kwa kuonyesha nia ya dhati ya kuendeleza michezo na elimu kupitia kampeni yake ya kuchangia jamii inayoitwa ‘Be Kidotified’.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uwanja wa mpira wa pete uliojengwa kwenye shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani kupitia kampuni ya Kidoti, Mkuu huyo wa wilaya alisema Tanzania ina wajasiriamali wengi wenye nafasi zaidi ya Jokate lakini mpaka sasa hawajafanya jambo lolote kwenye jamii zao.
“Jokate amebarikiwa na Mwenyezi Mungu, ameamua kugawana kile anachopata na jamii, mimi nilisoma hapa Jangwani na uwanja wetu wa michezo ulikuwa Gymkhana, Jokate amefuta safari ya wanafunzi kwenda huko, anastahili kupongezwa,” alisema Mjema.
Jokate naye alisema kuwa ameamua kuchangia maendeleo ya michezo kupitia Kidoti Brand hasa katika shule ambazo ni kiini cha michezo na elimu hapa nchini.
“Serikali ya awamu tano imedhamiria kuondoa changamoto nyingi kwenye elimu ila mimi nimeamua kuanzia huku kwenye michezo ambako huchangia ufaulu darasani na uibukaji wa vipaji ambavyo vitawawezesha kujiajiri,” alisema Jokate.
Blogger Comment