
WATU wawili wamepoteza maisha mkoani Kilimanjaro katika matukio mawili tofauti, likiwemo la abiria wa basi la Dar Express kuruka dirishani na kukanyagwa kichwani na gari hilo na kupoteza maisha papo hapo.
Akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa, alisema tukio hilo lilitokea saa 5:00 usiku wa Agosti 2 mwaka huu, katika barabara ya Moshi-Arusha eneo la Njiapanda ya KIA.
Alisema basi lilipofika eneo hilo, abiria aliyekuwa kwenye basi hilo aliruka dirishani na kukanyagwa na basi hilo na kufa papo hapo.
Kamanda Mutafungwa alisema basi hilo mali ya Kampuni ya Dar Express, lenye namba za usajili T 142 CDQ lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Arusha, likiendeshwa na Hassan Ismail (42).
Alimtaja marehemu kuwa ni Godbess Sawe (42) mkazi wa Ubungo Kibangu, Dar es Salaam, ambaye alikuwa amekaa sehemu ya dirishani katika basi hilo na aliruka wakati basi likitembea.
Mutafungwa alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, ambapo Jeshi la Polisi linamshikilia dereva wa basi hilo kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.
Katika tukio la pili, mkazi wa kijiji cha Uparo kilichopo kata ya Kirua Vunjo Kusini wilaya ya Moshi, Rose David (44) amekufa baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kuteketea kwa moto.
Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea saa 5:00 usiku, Agosti 2 mwaka huu, baada ya kibatari kuangukia kwenye tenga la nguo, kusababisha moto mkubwa ulioteketeza nyumba na mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba hiyo, ambapo hadi sasa thamani yake haijafahamika.
Blogger Comment