Asasi zinazotetea Ushoga zachunguzwa

SERIKALI inazichunguza asasi za kiraia zenye mwelekeo za kuunga mkono ushoga na ndoa za jinsia moja na zitakazobainika zitachukuliwa hatua kali.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe wakati akizungumza na uongozi wa asasi ya Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP) ofisini kwake Dar es Salaam.

Alizitaka asasi hizo kutokubali shinikizo kutoka kwa nchi zinazowapa misaada zenye nguvu kiuchumi za kutaka nchi zinazoendelea na asasi hizo zikubali ushoga na ndoa hizo za jinsia moja kama sehemu ya haki za binadamu ili kuendelea kupata misaada kutoka kwao.

“Nchi hizo zimekuwa zikitoa shinikizo kwa nchi zetu na hasa asasi nyingi zikizitaka zikubali ushoga na ndoa za jinsia moja, nazichunguza asasi zote za kiraia zenye mwelekeo huo na tukibaini mapungufu hayo tutazichukulia hatua kali za kisheria, uchafu na upuuzi huo wa wazungu, ubaki hukohuko kwao,” alisisitiza.

Waziri Mwakyembe alionya kuwa nchi ikilegeza kamba katika suala hili, “tutashinikizwa baadaye kufunga ndoa na wanyama wa kufungwa kwamba nayo ni sehemu ya haki za binadamu”.

Dk Mwakyembe amezitaka asasi hizo zisiyumbishwe na misaada kutoka nje yenye mwelekeo huo wa kukinzana na mila, desturi, utamaduni, imani za Watanzania, sheria na Katiba ya nchi.

Alisema serikali inaunga mkono juhudi za asasi mbalimbali za kiraia kama vile TGNP za kuelimisha jamii na kutetea haki za watoto, wazee, wanawake, walemavu na makundi mengine maalumu yanayostahili fursa na haki sawa katika jamii, lakini haitazivumilia asasi ambazo zinaenda kinyume na maadili na kukiuka sheria na taratibu ambazo nchi imejiwekea.

“Serikali inaunga mkono kazi zinazofanywa na asasi za kiraia nchini, lakini niweke wazi kuwa hatutazivumilia asasi za kiraia zinazoyumbishwa na misaada kutoka nje na kujihusisha na vitendo ambavyo vinakiuka maadili, taratibu na sheria za nchi ambazo zipo kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amon Mpanju, alisisitiza umuhimu wa asasi za kiraia kuisaidia serikali kwa kupeleka kwenye jamii ujumbe sahihi wenye mafundisho, badala ya kusubiri kukosoa tu na kuzitaka asasi za kiraia kuacha kuunga mkono hoja za ushoga kwa kishawishi cha fedha wanazopewa kutoka kwa wafadhili wao.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment