Waziri Mkuu Aongoza kikao cha wadau kujadili utekelezaji wa Serikali kuhamia dodoma ....... Awapa siku 14 wakamilishe na kumkabidhi mpango kazi wao


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia siyo siasa kama watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili na kwamba Serikali inakamilisha eneo la kisheria juu ya uamuzi huo.

“Hapa tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa pamoja na hakuna namna nyingine kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka niwahakikishie kwamba hii siyo siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo tu la kisheria juu ya uhamishaji wa makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii itapitishwa,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai 26, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, Serikali za mitaa, viongozi wa dini, wajasiriamali, wazee wa mji huo, wasafirishaji, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi za elimu, za kifedha na watoa huduma mbalimbali katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.

Waziri mkuu ambaye aliitisha kikao cha kazi na wadau hao mjini Dodoma, ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake wakae na kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma.

Pia ametoa siku 14 kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma kukamilisha mpango kazi wao na kumkabidhi mapendekezo yao ili yaweze kuingizwa kwenye mpango mkubwa wa Serikali kuu.

“Uongozi wa Mkoa, ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais TAMISEMI usimamie na kuyaratibu majukumu haya. Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna mtakavyoyatekeleza. Naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi yote niliyoyataja,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema chimbuko la uamuzi wa kuhamia Dodoma kuifanya makao makuu ya Serikali lilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo imeendelea kudumu katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 chini ya Ibara ya 151.

“Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na viongozi wengine wote wa Chama kwa  kusimamia  ndoto ya Baba wa Taifa ya kuhamishia  Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa wananchi wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa ujumla, amesema.

Akiweka msisitizo juu ya kazi kubwa inayowakabili viongozi hao, Waziri Mkuu amesema masuala yanayotakiwa kufanyika kuanzia sasa ni pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha eneo la makazi ya Serikali Kuu litakalotumika kwa ofisi za wizara na taasisi zake, makazi ya watumishi na huduma za biashara elimu na taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinakamilika kwa haraka na linakuwa tayari kwa matumizi.

“Natambua kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na inahitaji jitihada za pamoja. Hivyo kila taasisi na mtu mmoja mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa tunajipanga vizuri na kuweka mazingira ya ujio wa Serikali katika maeneo yote muhimu,” amesema.

Amezitaka Mamlaka za Mipango Miji na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo mmoja wa upatikanaji wa viwanja ambao utajulikana na kila mmoja, utakuwa wazi usio na urasimu. “Mfumo huu wa viwanja uwekwe kwenye mfumo wa kompyuta na uuzaji wa viwanja hivyo uwe wa kieletroniki kuepusha udanganyifu kutoka kwa madalali,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ameonya CDA na Manispaa zisibadili ramani ya mipango miji iliyokwishawekwa awali kama vile maeneo ya wazi kutumika tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na akaagiza maeneo hayo yote yarejeshwe na kufufuliwa.

“Natambua katika makazi hapa Dodoma kulitengwa maeneo ya vituo maalum vijulikanavyo kama D Centers kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali. Cha ajabu sasa kuna magenge, groceries na sasa naagiza kwa hadhi ya Makao Makuu haya maeneo sasa yatumike kuwekeza maduka makubwa (shopping malls) ambamo huduma zote mbalimbali hupatikana,” amesema.

Ameitaka Manispaa iboresha usafi wa mazingira na bustani zake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kuzitunza. Pia ameitaka manispaa ya mji huo ishirikiane na TANROADS kuboresha barabara zote za mitaa na taa za barabarani mji ukae kisasa, na usalama uwe bora zaidi.

“Eneo jingine muhimu ni Manispaa na CDA kuhamisha makundi mbalimbali ya wafanyabiasahra na huduma za masoko yasiyo rasmi na kuyapa maeneo yaliyo rasmi na bora zaidi.  Hii ni pamoja na maeneo ya maegesho ya bajaji, bodaboda, taxi na daladala. Pia mazingira ya Stendi Kuu yaboreshwe, vyoo vya kulipia pia vijengwe katikati ya mji,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa majengo (TBA) waorodheshe majengo yote ya Serikali na taasisi zake yanayotumika kwa sasa na yasiyotumika, “Nataka muyawekee utaratibu maalum wa matumizi yake ili tupate kujua yanayoweza kutumika kwa muda kwa baadhi ya wizara na taasisi zake. Hii ni pamoja na jengo jipya la Mkuu wa Mkoa, linaloendelea kujengwa.”

Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.

JUMANNE, JULAI 26, 2016.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment