Issa Mnally na Richard Bukos, UWAZI
DAR ES SALAAM: Kufuatia mauaji ya kupigwa risasi kwa askari wa kitengo cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Alex Naiman Njau katika makutano ya Barabara za Rose Garden na Bagamoyo jijini Dar, Ijumaa usiku, Uwazi limezama na kuibuka na undani wa tukio hilo la kinyama.
KUTOKA ENEO LA TUKIO
Baadhi ya mashuhuda waliozungumza na gazeti hili eneo la tukio, walisema kulikuwa na lengo maalum la wauaji hao, kwani kabla ya kutekeleza kitendo hicho, walisimama kwa muda mrefu ng’ambo ya barabara hiyo, wakiwatazama askari hao waliokuwa wamekaa kwenye kibanda chao kilicho kando ya barabara, nje ya jengo lenye ofisi za posta.
WATU WALIJUA NI BODABODA
“Jamaa mmoja yeye alikaa juu ya pikipiki aina ya Boxer upande wa pili wa barabara, mwenzake alisimama pembeni yake. Kila aliyemuona alijua ni bodaboda anasubiri wateja. Baadhi ya wateja walipofika, aliwajibu anasubiri mteja mwingine.
“Basi, walisimama pale kwa muda mrefu na wale matrafiki walikuwa kwenye kibanda chao wakiendelea na majukumu yao. Ilikuwa kama saa mbili hivi usiku, lakini ghafla tulisikia mlio wa risasi na tukamuona huyo trafiki akianguka huku mwenzake akitimua mbio,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Shuhuda mwingine aliliambia Uwazi kuwa, watu hao waliwafuata trafiki hao kama wenye kuhitaji msaada wa matatizo ya barabarani, lakini ghafla walitoa bastola na kuwaweka chini ya ulinzi, kitendo ambacho marehemu hakukikubali, kwani alianza kupambana nao na kufanikiwa kumuangusha mmoja kitendo kilichompa upenyo yule trafiki mwenye mbwembwe, Konstebo Ashraf kukimbia.
Kuna taarifa pia kuwa maafande hao walikataa kutii amri ya wauaji hao ya kuweka chini kila walichokuwa nacho na ndipo pakatokea purukushani ambapo Ashraf alifanikiwa kumuangusha kwa teke mmoja wa wauaji hao aliyekuwa na bastola lakini kwa vile yeye hakuwa na silaha, baada ya kupata upenyo alikimbia na kumuacha Njau akigalagala naye kutaka kujiokoa.
Ndipo akiwa kwenye harakati za kujitetea, wauaji hao walimuwahi kwa kumpiga risasi mbili za kifuani ambazo zilitokea mgongoni.
Uwazi, Jumamosi iliyopita, lilifika kwenye msiba wa trafiki huyo, Kambi ya Polisi, Kunduchi jijini Dar alipokuwa akiishi marehemu na familia yake na kuzungumza na ndugu na jamaa waliokuwepo.
Uwazi lilianza kuzungumza na mpwa wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Anna Tillya ambaye alisema:
“Jamani mimi nashindwa kuamini kilichotokea, sijui kama ni visasi, ujambazi au ni kitu gani kwani siku moja kabla tukio niliongea na marehemu kwenye simu, hakuonesha dalili kwamba ana jambo la kupambana na wabaya wake.
“Katika maisha yake, mjomba hakuwahi kutuambia kama alikuwa na bifu au mgogoro na mtu yeyote na mara nyingi alikuwa mkimya lakini alipenda kuongea kwa kusisitiza. Ukweli kama kulikuwa kuna mtu ana bifu naye sisi hajawahi kutuambia.”
MKE WA MAREHEMU AISHIWA NGUVU
Gazeti hili lilitaka kuzungumza na mke wa marehemu ili kujua kama kuna jambo ambalo huenda analihusisha na tukio hilo, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kutokana na mjane huyo kuishiwa nguvu na kushindwa kuongea chochote zaidi ya kila wakati kulitaja jina la mume wake.
TRAFIKI MMOJA NA UWAZI
Likiwa msibani hapo, Uwazi lilizungumza na trafiki mmoja ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu, yeye alikuwa na haya ya kusema:
“Unajua kazi yetu sasa hivi inatisha sana, maana tumekuwa tukiuawa kwa kupigwa risasi na wakati mwingine kugongwa makusudi, yaani kusema kweli tuna hofu kubwa sana, kazi yetu imekuwa ya shaka. Hasa sehemu yenye mataa ndiyo hatari zaidi.”
Trafiki mwingine aliyeongea na gazeti hili msibani hapo alisema:
“Hili tukio limetuchanganya sana maana huenda vikawa ni visasi vya mambo ya mapenzi, kwa kuwa kama ni ujambazi, sasa matrafiki walikuwa na kitu gani cha thamani ya kuwavamia na kuwaua?
“Siku moja marehemu aliwahi kuniambia kuwa, kuna mtu mmoja aliwahi kumtuhumu kuwa na ukaribu na mkewe, akamwambia siku si nyingi atamwonesha jeuri yake, lakini mwanamke mwenyewe, marehemu alikuwa hamjui jina wala sura, aliamini mwanaume huyo alimfananisha yeye. Sasa isije kuwa ndiyo kisasi cha kumwambia ataona.”
“Lakini pia hapo naona kuna masuala binafsi au ya kikazi, kwani mchana alinipigia simu, akaniambia kuna mzee mmoja alipita eneo hilo akamkamata kwa makosa ya gari lake, mzee akasema yeye ni mtu mkubwa, amuachie lakini hakumwachia, akamwandikia faini, akamwambia ataona licha ya kwamba alimwandikia. Haya mambo yakifuatiliwa kwa umakini kila kitu kitabainika.”
SIMU YA TRAFIKI MWENYE MBWEMBWE YASHIKILIWA
Uwazi lilimtafuta afande Ashraf ambaye anasifika kwa kuongoza magari kwa mbwembwe ambaye pia alipambana na wauaji hao kabla ya kuwachoropoka na kujiokoa lakini zoezi hilo liligonga mwamba na simu yake haikuwa hewani ikisemekana inashikiliwa na polisi katika Kituo cha Oysterbay, Dar kwa uchunguzi zaidi.
KAMANDA WA POLISI
Uwazi lilizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, SACP Christopher Fuime ambaye alisema tukio hilo lina mkanganyiko mkubwa lakini jeshi hilo linaendelea na upelelezi. Mpaka sasa tunamshikilia mtu mmoja kufuatia mauaji hayo lakini uchunguzi zaidi unaendelea. “Chanzo cha tukio hilo mpaka sasa bado kinatuchanganya ndiyo maana kazi ya kuwakamata wahusika inakwenda taratibu kwa kuwa inahitaji sayansi ya hali juu lakini tutahakikisha tunafanya hivyo.
Ingekuwa chanzo kinafahamika kama ni mgogoro fulani ingekuwa rahisi kuwakamata wahusika lakini katika hili jambo hakuna kinachofahamika ndiyo maana nimekuambia linahitaji uchunguzi wa kisayansi,” alisema Fuime.
Mei 19, mwaka huu, trafiki mwingine aliyekuwa akisikika asubuhi kwenye Kipindi cha Barabara Zetu cha Redio One Stereo, Sajenti Ally Salum Kinyogoli naye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake, Chatembo, Kata ya Mwandege, Mkuranga, Pwani mbele ya mtoto wake mwenye miaka 11.
Mwili wa marehemu unasafirishwa leo kupelekwa mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Blogger Comment