WAKATI suala la serikali kuhamia mkoani Dodoma likiwa dhahiri zaidi kila siku moja inayoongezeka, Rais John Magufuli ametangaza kuuza majengo ya wizara Dar es Salaam, mara atakapohamia yeye katika makao makuu hayo ya nchi.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara mkoani Singida, katika siku ya kwanza ya ziara yake itakayomfikisha mikoa minne, Rais Magufuli alisema atahakikisha anauza baadhi ya majengo hayo kwa mnada, ili wale wasiotaka kuhama, wahame kwa lazima.
Mbali na Singida, mikoa mingine atakayotembelea katika ziara hiyo aliyoanza jana ni Tabora, Shinyanga na Geita, ambako atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Katika mikutano hiyo, Rais Magufuli anatarajiwa kushukuru wananchi kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo.
Majengo mazuri
Katika tangazo hilo, Rais Magufuli amesema majengo atakayoanza nayo, ni yale yanayotazama bahari; ambayo ndiyo mazuri zaidi, yenye mwonekano mzuri kutoka ofisini.
“Atakayeng’ang’ania kubaki huko, ajue hana kazi wala mshahara. Hatuwezi kuendelea kukaa miaka hamsini tunaimba tu kuhamia Dodoma, wakati hatutekelezi uamuzi wetu hadi wengine wameshatangulia mbele za haki,” alisema.
Alisema anajua akiitisha zabuni ya ofisi hizo, wateja watayakimbilia kwa wingi, hivyo wataong’ang’ania kubaki Dar es Salaaam, watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe.
Uamuzi huo wa serikali kuhamia Dodoma japo ni wa siku nyingi na utekelezaji wake ulikuwa ukifanyika kidogokidogo kwa baadhi ya wizara na ofisi nyeti kujenga majengo yake katika mji huo, lakini hivi karibuni umepata kasi ambayo haijawahi kupatikana, baada ya Rais Magufuli kutangaza kuhakikisha serikali yote inahamia Dodoma kabla ya 2020.
Tamko hilo la Rais Magufuli lililotolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM wiki iliyopita na kurejewa katika Sikukuu ya Mashujaa mwanzoni mwa wiki hii, liliungwa mkono mara moja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye alitangaza kuharakisha umaliziaji wa ujenzi wa nyumba yake, ili ahamie katika mji huo Septemba mwaka huu.
Wizara zenyewe
Baadhi ya mawaziri waliohojiwa na vyombo mbalimbali vya habari, walikaririwa wiki hii wakisema kuwa suala hilo halina mjadala ni la kutekeleza mara moja.
Mbali na waliohojiwa, mawaziri na watendaji wakuu wengine serikalini, walitangaza muda maalumu kwa watendaji wao kuanza kuhamia katika mkoa huo.
Miongoni mwa mawaziri hao, ni pamoja Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, ambaye naye wiki hii alikutana na vyombo vya habari na kutangaza kuwa baadhi ya watendaji wa wizara hiyo, wataanza kuhamia Dodoma kuanzia wiki ijayo.
Dk Tizeba alikaririwa akisema tayari watendaji wa wizara hiyo wanaotakiwa kuhamia Dodoma wameanza kufanya maandalizi ya safari.
Wakati Tizeba akitajwa kuwa waziri atakayewahi kuhamia pamoja na wizara yake Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, naye alitaja utaratibu wa kuhamia Dodoma.
Profesa Ntalikwa aliwataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo, kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma na kuwa wametekeleza agizo hilo ifikapo Septemba, mwaka huu, muda ambao Waziri Mkuu naye anatarajiwa kuwa Dodoma.
Agizo hilo la Wizara ya Nishati na Madini, liliwekwa katika waraka uliotolewa na watendaji na nakala yake kutumwa pia kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Madalali viwanja
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana jana alipiga marufuku uuzaji wa viwanja ndani ya mji wa Dodoma, baada ya kubaini kuwepo kwa kundi la madalali kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo kutoka Dar es Salaam kuhamia katika mji huo.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Rugimbana alisema amepiga marufuku uuzaji huo mpaka baada ya siku 14 baada ya Waziri Mkuu kuhamia Dodoma, wakati Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ikishirikiana na kikosi kazi kilichoundwa na serikali chini Ofisi ya Waziri Mkuu, watakapotoa utaratibu.
Alisema kumezuka kundi la madalali kutoka mikoa mingine walioanza biashara ya viwanja na mashamba bila kufuata utaratibu na kanuni, hivyo uongozi wa mkoa wamezuia suala hilo, kwani linaweza kuvuruga na wananchi watakaotoa viwanja kwa madalali hao itakuwa imekula kwao.
Lengo la serikali kwa mujibu wa Rugimbana, ni kuhakikisha kila Mtanzania mahali alipo anaweza kupata kiwanja huko alipo. Rugimbana alisema mji wa Dodoma ulipangwa siku nyingi; kila eneo na matumizi yake ya ardhi hivyo kuwataka wanaotaka kununua ardhi kuwa makini, ili wasiuziwe maeneo ya makaburi au masoko.
“CDA watafanya kazi vizuri na Mtanzania yeyote anayeweza kununua eneo huko alipo bila ya kuja Dodoma na atakuja hapa wakati wa kukabidhiwa hati na kiwanja,” alisema.
“Ndani ya siku 14 tutatoa maelekezo namna ya kupata viwanja Watanzania wawe watulivu utaratibu mzuri unakuja na hakuna Mtanzania ambaye anataka kujenga Dodoma atakosa kiwanja.
“Mtu anayetaka, asubiri na mfumo utakuwa wazi kwa kila mmoja na utaratibu wa kisheria utafuatwa,” alisema.
Miji miwili
Pamoja na hayo Mkuu huyo wa Mkoa alisema baada ya wizara mbalimbali kuhamia Dodoma, maeneo ya mjini yatakuwa kwa ajili ya biashara na mji wa serikali utakuwa kuanzia Ihumwa hadi Chamwino Ikulu ambapo zitajengwa ofisi za serikali.
Kuhusu ofisi zitakazotumiwa na wizara mara baada ya kuhamia Dodoma mwaka huu, Rugimbana alisema watatumia ofisi zilizopo mjini kabla ya ujenzi katika eneo la Ihumwa ambako kutakuwa na ofisi hizo za muda.
‘’Wizara zikija Dodoma zitaanza kutumia ofisi zilizopo ambazo zilikuwa zikitumika awali kabla ya ujenzi wa ofisi katika eneo la Ihumwa kukamilika,’’ alisema.
Alisema sababu ya kupeleka mji wa kiserikali Ihumwa, ni kuondoa msongamano wa magari kama ilivyo katika jiji la Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa kutakuwa na miji miwili; mji wa serikali utakaokuwa Ihumwa na mji wa kibiashara utakaokuwa katika Mji wa Dodoma. Aliwatoa hofu watumishi wa wizara mbalimbali watakaohamia Dodoma kuwa kuna nyumba za kutosha za wao kuishi.
‘’Dodoma tuna nyumba nyingi sana, watumishi hawawezi kukosa nyumba, tutawakodishia hata nyumba binafsi ili waishi,’’ alisema.
Blogger Comment