Hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe, imelalamikiwa na Festo Loya, ambaye alisimamiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye shauri la jinai namba 65/2015, lililomhusisha mtuhumiwa Petro Gembe.
Akizungumza na JAMHURI, Loya anasema alipeleka shauri hilo mahakamani kutokana na kitendo cha kuvamiwa nyumbani kwake, na kuporwa mali huku pia mke wake akifanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kubakwa na kundi la watu aliowafahamu.
Mtuhumiwa huyo alihukumiwa kifungo cha nje kutokana na sababu ya umri wake, na kwamba hatatakiwa kufanya kosa la aina yoyote katika kipindi cha miezi 12. Alikuhukumiwa kulipa kiasi cha Sh milioni 69.35 kama sehemu ya fidia ya wizi wa mifugo na fedha zilizoibwa.
Anasema, kumekuwa na matendo ya kujirudia rudia ya mke wake kutekwa na kupelekwa kusikojulikana, huku watekaji hao wakilazimisha kumuoa kwa nguvu. Majaribio hayo yamefanyika zaidi ya mara tatu. Pamoja na hukumu hiyo kutolewa, anasema mtuhumiwa hajamlipa chochote, hukumu ilisomwa Machi 30, 2016.
“Tukio la kwanza lilitokea Mei 2015, huko Magogoni kitongoji cha Nyagwa, Morogoro. Mke wangu alitekwa na kupelekwa Rukwa, watekaji walikuwa wakimbaka siku zote katika kipindi cha miezi miwili,” anasema Loya kwa masikitiko.
Loya ambaye ni kijana kutoka jamii ya wafugaji, anasema kumekuwepo na malumbano mengi kutoka kwa waliokuwa wakitamani kumuoa mkewe. Anasema kundi hilo limekuwa likijinasibisha na kugawa fedha (rushwa) katika taasisi ambazo yeye amekuwa akipeleka mashtaka yake.
Naye mke wa Loya, Dang’au Geida anasimulia namna alivyotoroshwa kutoka Morogoro mpaka Rukwa, na jinsi alivyowasiliana na mumewe na wazazi wake kujinasua kutoka katika mikono ya wabakaji.
Anasema baada ya kutoroshwa alifichwa sehemu ambayo yeye hawezi kuikumbuka. Alikaa mahala hapo kwa siku tatu hivi kabla ya kupelekwa katika Kijiji cha Pangala kilichoko Sumbawanga, Rukwa.
“Nilitekwa na kuchukuliwa na hao wabakaji…nikiwa huko Rukwa nilikuwa nimewekewa walinzi watatu, ambao wao kazi yao ilikuwa kunichunga mimi tu. Lakini siku moja nikafanikiwa kupata simu na kumtumia baba yangu ujumbe mfupi wa maneno,” anasimulia Dang’au.
Anaongeza, “Baada ya baba yake kufuatilia na kumpata hakuhitaji masuala ya kesi…baba alimshauri mume wangu kwamba kwa kuwa nimepatikana basi hiyo ilikuwa inatosha, maana nilikuwa kusikojulikana kwa miezi mitatu. Miezi hiyo yote nikiwa nalazimishwa kufanya mapenzi.”
Kisa cha shauri hilo la Jamhuri dhidi ya Petro Gembe, ni mwendelezo wa vurugu za kutekwa na kutoroshwa kwa Dang’au. Loya anasema walikuja kikosi cha vijana tisa wakiongozwa na mtuhumiwa.
Anasema katika hoja zilizopelekwa Mahakamani kuthibitisha ushiriki wa mtuhumiwa katika kupora mifugo pamoja na kitendo cha kumbaka Dang’au, ni kwamba Petro Gembe (75) mkaazi wa Magogoni katika wilaya ya Morogoro, Juni 24, 2015 mtuhumiwa alikuwa katika Kijiji cha Kimalamisale, wilayani Kisarawe.
“Katika tarehe iliyotajwa mtuhumiwa aliiba ng’ombe 53 waliokadiriwa kuwa na thamani ya Sh milioni 21, pamoja na kuiba pesa kiasi cha Sh milioni 48.35. Thamani ya mali zote ni Sh milioni 69.35,” anasema Loya.
Loya anasema Gembe pamoja na vijana wake walifanya vurugu huku wakitumia silaha za jadi, walifanikiwa kuchukua mifugo pamoja na kuondoka na mke wake.
“Nakumbuka Juni 23, nilipata taarifa kwamba Petro Gembe alipanga kutuma watu wake ili waje kumchukua mke wangu, aliyeniambia alisema watu hao wangekuja na silaha…baada ya kuvamiwa nilitoa taarifa kituo cha Polisi cha Kwala, nilipatiwa RB ili nikamkamate mtuhumiwa wangu Morogoro,” anasimulia.
Juni 26, 2015 alitoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Mvuha, Morogoro anasema alipewa askari polisi wapatao saba wamsaidie kufahamu alikokuwa mtuhumiwa wake na kumkamata. Anasema kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa katika Kijiji cha Nyangwa huko Morogoro.
“Mtuhumiwa alipofikishwa kituo cha Polisi cha Mzenga, Kisarawe aliachiwa na nikaenda kulalamika kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya na mtuhumiwa wangu alikamatwa tena,” anasema Loya.
Pamoja na ushahidi wa kupora ng’ombe, fedha tasilimu na mke wa mtu, bado hakimu aliyeendesha kesi hiyo alimpa Mzee Gembe kifungo cha nje kinyume na sheria inayosimamia makosa ya ubakaji na wizi wa kutumia silaha.
Gembe aliamuriwa kulipa hiyo fedha baada ya kukiri mahakamani kuwa ni kweli alichukua hao ng’ombe, fedha tasilimu na mke wa Loya. Hata hivyo, hadi sasa pamoja na hukumu ya kumtaka alipe wastani wa Sh milioni 69, hadi leo hajalipa na anatamba mitaani kuwa hakuna wa kumfanya chochote.
Akizungumza na JAMHURI, Hakimu aliyeshughulikia shauri hilo Hamis Ali Salum, anasema ni kweli jambo hilo lilikuwa chini yake. Hakimu akalitaka JAMHURI lifunge safari kwenda Kisarawe kwa ajili ya mazungumzo.
Hakimu Salum anasema, “Hayo ni masuala ya ofisi na sio binafsi, hatuwezi kuongea kwenye simu. Hata hivyo huyo bwana kama hakuridhika na hukumu asilalamike, akakate rufaa katika mahakama husika ili apate haki yake,”
Blogger Comment