
Rais amesema, anamjua kila mmoja aliyemteua na kuna wakati alilala saa nane au saa tisa usiku akifanya kazi kuwachunguza. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, wakati anafanya kazi hiyo alimuomba sana Mungu asimuonee mtu na asimpendelee mtu.
“Kila mmoja nimemchambua kweli kweli, ndiyo maana mimi sitembei” amesema Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya wakurugenzi hao kula kiapo cha uadilifu wa uongozi wa umma.
Amewataka viongozi hao wakafanye kazi na hataki siku moja aamini kwamba alifanya makosa na ikitokea hivyo ataumia sana.
“Ukifuatilia yale yaliyokuwa yanazungumzwa unasema eeh nimekosea nini, kumbe aah, Mungu awabariki sana” anasema Rais na kuwataka wakamalize kero mbalimbali kwa wananchi zikiwemo kodi zisizo muhimu.
“Mkawe watatuzi wa matatizo badala ya kuwa watengenezaji wa matatizo kwenye maeneo yenu”amesema Rais Magufuli na kuwataka wakashirikiane na viongozi wengine kuwasaidia Watanzania hasa wananchi wanyonge.
Dk Magufuli amesema, hakuna aliyepenyeza jina lake likapita, yeye ndiye anayewafahamu na ndiye aliyewateua. Amesema, yeye ana imani nao, serikali ina imani nao na anaamini watatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nataka ninyi mkawe mitume wazuri kwa wananchi, imani izae imani” amesema Rais na kuwaeleza viongozi hao kuwa, hawahitaji kushangiliwa, wananchi watawashangilia wakitekeleza vizuri wajibu wao.
Amewaeleza kuwa, watapata majaribu mengi yakiwemo kutoka kwa wafanyabiashara na wanasiasa hivyo wawe imara, wasimamie sheria na watumie vizuri fedha za umma kutekeleza miradi na kutatua kero zinazowakabili wananchi.
“Tuliahidi kutatua kero kwa wananchi, hatukuahidi kutengeneza kero kwa wananchi” amesema.
“Nimewateua mimi, Mkitimiza maadili yenu hakuna atakayekufukuza” amesema Rais Magufuli katika tukio hilo lililohudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa serikali.
Blogger Comment