SIKU moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza nia ya kufanya mikutano ya hadharani nchini kote kuanzia Septemba Mosi kutokana na sababu mbalimbali, taasisi na wadau mbalimbali wamelaani mpango huo.
Akizungumzia hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema amepokea kwa masikitiko makubwa tamko hilo, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijitokeza na kulaani mpango huo.
Wengine waliopinga mpango huo ni wasomi wakiwemo Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayejipambanua katika siasa za upinzani, aliyewahi kuwa mwanachama wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo na wachambuzi wa Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Benson Bana na Dk Bashiru Ally.
Msajili vyama vya siasa alaani
Akizungumzia tamko hilo la Chadema, Jaji Mutungi alisema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, kuudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Alisema kimsingi Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 kifungu (2) (c) inakataza chama cha siasa kutumia au kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake kisiasa.
Alisema aidha kifungu cha 9 (2) (f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu wanachama au viongozi wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha au kupelekea kutokea uvunjifu wa amani.
Alisema pia kanuni ya Maadili ya Vyama vya Siasa, Tangazo la Serikali namba 215, linakataza chama cha siasa kutumia lugha za matusi, kashfa, uongo na uchochezi.
Alisema Kanuni ya 5 (1) (d) inakitaka chama cha siasa kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni uongo, kuhusu mtu yeyote au chama cha siasa chochote. “Hivyo tamko la Chadema ni ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Aidha, hii si mara ya kwanza kwa Chadema kutumia lugha za namna hii za kuhamasisha uvunjifu wa amani.
“Natumia fursa hii kukemea tamko hilo hadharani, kwa mujibu wa kanuni ya 6 (2) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, pia nawaasa Chadema wasiendeleze tabia hii,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema dhamana aliyopewa kama Msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa kazi yake ni kuviasa vyama vyote vya siasa vitimize wajibu wao kwa weledi kama taasisi za kisiasa.
“Ni vyema viongozi wa vyama vya siasa wakaonesha taswira stahiki ya wanasiasa wakomavu, au vyama vya siasa vya kutolea mfano ndani na nje ya mipaka yetu, kwa kuzingatia sheria za nchi katika kuendesha shughuli za kisiasa. “Vyama vya siasa viepuke vitendo, kauli au matamshi yenye mlengo wa kusababisha uchochezi au kufarakanisha umma na serikali yao. Navisihi kuzingatia utaratibu wa mawasiliano kwa mujibu wa sheria zilizopo, aidha uvumilivu wa kisiasa katika azma za kudumisha ukuaji wa kidemokrasia nchini haukwepeki,” alisema Jaji Mutungi.
CCM wajibu mapigo
Katika hatua nyingine CCM imeionya Chadema kuacha kupotosha umma na kutaka kuwaaminisha wananchi uongo wanaoutunga ili kujaribu kupata wafuasi.
Aidha, imewataka Watanzania kupuuza maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chadema kwa kuwa ni ishara ya kuchochea uvunjifu wa amani, huku ikiwataka viongozi hao wanaoshinikiza maandamano kuandamana na familia zao.
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema Dar es Salaam jana kuwa tamko lililotolewa na Chadema la kupanga kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, limejaa uongo na ubabaishaji na linaonesha kuwa wapinzani wamekosa ajenda na njia pekee wanayoona inafaa ni kutunga utapeli, uongo na uzushi.
Alisema kimsingi hoja walizotumia kufikia uamuzi wao bila kuzirudia zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri.
Alisema kwa mfano chama hicho kimekuwa kikidai serikali imezuia mikutano yote ya vyama vya siasa huku wakijua jambo hilo si kweli. “…Wamekuwa wakisema hivyo huku wakijua kuwa ni uongo kwani serikali haijazuia mikutano. Kwenye majimbo wabunge wao wako huru kufanya shughuli zao, tumeona wabunge wakifanya mikutano kwenye majimbo ikiwemo wa upinzani,” alisema Ole Sendeka.
Alisema vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa Katiba si kosa na wala si jambo ambalo limezuiliwa na ndio maana imeshuhudiwa vyama vya siasa vikifanya mikutano yao ya kikatiba bila tabu.
Ole Sendeka alisema jambo lingine ambalo ni hoja za uongo na uzushi ni kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya kidikteta, na alihoji udikteta wanaousema Chadema ni upi? “Ni huu wa kushughulikia watumishi hewa, ni huu wa kuwabana wakwepa kodi, ni huu wa kupunguza na kudhibiti safari za nje, ni huu wa kubana matumizi ya serikali, ni huu wa kufukuza wazembe na wabadhirifu kazini? “Hivi udikteta huo ni huu wa kushughulikia mafisadi na mpaka kuanzisha Mahakama yao?” Alihoji Msemaji huyo wa CCM.
Alisema CCM inaamini Watanzania wengi wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli na serikali yake, lakini kama hatua hizo Chadema inaona ni udikteta bila shaka wao ni sehemu ya mfumo mbovu na ndio maana wako tayari kuleta vurugu.
Wasomi UDSM wafunguka
Wakitoa maoni wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mkumbo, Dk Bashiru na Bana walikosoa mpango huo wa Chadema. Profesa Mkumbo alisema vyama vya siasa vina wajibu wa kulinda misingi ya demokrasia lakini pia vina haki ya kupigania kufanya shughuli za siasa ingawa si kwa mapambano.
Alisema ni muhimu vyama vya siasa kujenga amani ya nchi lakini akasema ni muhimu pia kwa Jeshi la Polisi kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu kupinga mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.
“Pande zote mbili yaani Jeshi la Polisi na vyama vya siasa vipeane nafasi kila mmoja, bila kuvuruga shughuli za maendeleo, kulindwa kwa demokrasia na kuiendeleza,” alisema Profesa Mkumbo.
Naye Dk Bashiru alisema kauli ya kufanya mikutano nchi nzima ni vyema ikafafanuliwa, kuhojiwa au kutafsiriwa na taasisi za kidemokrasia ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inasiamamia sheria za vyama vya siasa.
Alisema taasisi hiyo itoe ufafanuzi kwa kuzingatia sheria ili kuongoza kauli na vitendo vitolewavyo na vyama vya siasa katika kukuza demokrasia, pamoja na kuangalia matakwa ya wanasiasa ili isiwe ni kuvuruga misingi ya mamlaka.
Alisema hakuna mahali utaratibu, sheria na kanuni zinafuatwa kiholela, na kwamba uholela haujengi demokrasia bali ni chanzo cha chuki na hata kuumiza, hivyo yawepo mazungumzo ili kufikia muafaka na kama yupo asiyeridhika aende Mahakamani.
Blogger Comment