Hatimaye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye
amekuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa alikamatwa jana
katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea
Japan.
Baada ya Askofu Gwajima kukamatwa na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa
JNIA alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya
mahojiano akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.
Akizungumzia kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin
Otieno alisema askofu huyo aliwasili saa 2.45 asubuhi akitokea Japan kwa
kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
Otieno alisema mara baada ya kukamatwa alipelekwa katika Kituo Kikuu cha
Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam.
“Ni kweli tulimkamata Askofu Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada
ya kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na tulipomuhoji
alidai kuwa alikuwa nchini Japan,” alisema Otieno.
Mwanasheria wake Peter Kibatala alisema Gwajima alifika Kituo Kikuu cha
Polisi saa 4.45 asubuhi kwa mahojiano mafupi na aliruhusiwa kuondoka
baada ya kujidhamini yeye mwenyewe.
“Askofu Gwajima amehojiwa leo (jana) na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na
amejidhamini yeye mwenyewe, ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri
chochote kitakachoendelea,” alisema Kibatala bila kueleza mahojiano
yalivyokuwa.
Askofu Gwajima alikuwa anatafutwa na polisi tangu mwezi uliopita baada
ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti
yake akipendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kufikishwa mahakamani kwa
yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo sasa Rais John Magufuli
anayashughulikia kwa mtindo wa kutumbua majipu.
Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM
wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Rais Magufuli asipewe
uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu wa chama hicho na
kwamba hilo likifanyika basi Rais abadili katiba ili mstaafu huyo aweze
kufikishwa kortini.
Tangu ulipotolewa mkanda huo, makachero wa polisi wamekuwa wakipiga
kambi nyumbani kwa Askofu Gwajima kwa lengo la kumkamata lakini
hawakumpata.
Baadaye ilikuja kufahamika kwamba askofu huyo alikuwa amekwenda nje ya nchi lakini haikujulikana ni nchi gani.
Hata hivyo, baada ya kutafutwa na polisi, Gwajima kupitia wakili wake
Kibatala alisema atakaporejea nchini atakwenda moja kwa moja polisi kwa
ajili ya mahojiano.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amekuwa
akisisitiza kwamba jeshi litaendelea kumtafuta askofu huyo kwa
kushirikiana na polisi wa kimataifa, Interpol.
Blogger Comment