
MTU mmoja amekufa na wengine wawili kujeruhiwa wilayani Ukerewe, Mwanza baada ya pikipiki mbili kugongana.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 12.30 katika Kata ya Kagera mjini Nansio barabara ya Nansio - Bomani ambapo mmoja wa abiria wa pikipiki hizo alianguka chini na kupoteza maisha wakati akipelekwa hospitali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alimtaja aliyekufa kuwa ni Mashauri Nyanda (41) mkazi wa Igoma jijini Mwanza ambaye alifikwa na mauti baada ya kupata majeraha makubwa kichwani na pia kuvunjika ubavu wa kulia.
Alisema Nyanda alianguka akiwa amepanda kwenye pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Talwema Victor (20) yenye Usajili namba MC.147 AWE aina ya Honda ambayo iliigonga pikipiki yenye Usajili namba MC.331 AKE aina ya San-LG iliyokuwa ikiendeshwa na Dominick Maximilian (22).
Katika ajali hiyo, watu wengine wawili Magdalena Steven (16) ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili wa Shule ya Sekondari Bukongo na Baraka Samwel (22) walijeruhiwa na wanatibiwa katika Hospitali ya Nansio.
Kamanda Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kuongeza kuwa tayari Talwema amekamatwa na baada ya mahojiano atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema Talwema alikuwa katika mwendo kasi na kugonga pikipiki nyingine ndipo pikipiki hizo zilipoyumba na kuwaangukia watu waliokuwepo eneo hilo na kuwajeruhi.
Blogger Comment