RAIS John Magufuli, amemtaka Dk. Ali Mohamed Shein, kumpa tuzo Jecha Salim, mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, kutokana na kile alichokiita kazi nzuri aliyoifanya visiwani humo mwaka jana, kwa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana jioni, katika ziara yake ya kikazi visiwani Pemba. Wakati Rais Magufuli akichaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, Dk. Shein alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kufuatia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi mwaka huu.
“Nampongeza sana Jecha kwa kazi nzuri aliyofanya kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, na kwa kweli Dk. Shein kama kuna tuzo zako utakazotoa, naomba usimsahau kumpa na Jecha,” alisema Rais Magufuli.
Rai Magufuli pia alimtaka Rais huyo wa Zanzibar kumtaarifu yeye ili awashughulikie watu wote wanaomsumbua visiwani humo au wanaoonekana kumzidi nguvu.
“Rais Shein kama kuna mtu unaona anakusumbua wewe au anakupa tabu nijulishe mimi tu, hata dakika tano hazitapita nitamshughulikia,” ameeleza.
Kauli hiyo inakuja, ikiwa ni zaidi ya miezi kumi sasa tangu hali ya mahusiano baina ya wananchi wa Zanzibar iwe tete, tangu pale Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) alipotangaza kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Mahusiano hayo mabaya yamesababisha, wafuasi wa vyama vya CUF na CCM vyenye nguvu zaidi visiwani humo, kufikia hatua ya kusitisha ushirikiano katika shuguli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kutohudhuria misiba na kutonunua bidhaa za mtu wasiyeendana naye kiitikadi.
“Niombe vyombo vya ulinzi na usalama wafuatilie hao wanaokatakata na kuchoma karafuu washughulikiwe bila huruma. Atakayejaribu kuichezea amani, atacheza yeye tena mchezo asiojua kuucheza,” aling’aka Rais Magufuli.
Tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana visiwani Zanzibar, hali ya usalama imekuwa si ya kuridhisha.
Nyumba na mashamba ya karafuu yamekuwa yakichomwa moto, huku baadhi ya watu wakitiwa mbaroni na vyombo vya dola kwa tuhuma hizo
Blogger Comment