WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ametaka wakuu wa wilaya wastaafu ambao hawakuteuliwa katika kipindi cha awamu ya tano, kutosikitika na kukata tamaa kwa kukosa nafasi hiyo, badala yake waitumie fursa waliyonayo kujiendeleza zaidi.
Simbachawene pia amewahakikishia viongozi hao waliomaliza muda wao kuwa kwa mujibu wa Rais John Magufuli, mchakato wa mafao yao tayari umeanza kutekelezwa na muda wowote wataanza kulipwa mafao hayo.
Akifungua semina ya mafunzo ya ujasiriamali iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa wakuu hao wa wilaya pamoja na viongozi wengine wastaafu, Waziri huyo alisema ni jambo la kawaida kila uongozi mpya unapoingia madarakani kubadilisha timu yake ya kufanyia kazi.
Alisema pamoja na kwamba Dk Magufuli hakuwateua kuendelea na nyadhifa zao za ukuu wa wilaya, bado anawatambua na kuwaamini kwani wengi wamefanya kazi kubwa ya maendeleo katika maeneo yao.
“Nawahakikishia Rais bado ana vyeo vingi hapa leo mnazungumzia kustaafu, lakini inawezekana wengine wakateuliwa leo au kesho kushika nyadhifa zingine tena za juu zaidi. Wengi wa wakuu wa wilaya wastaafu bado ni vijana, bado taifa linawategemea,” alisema Simbachawene.
Aliupongeza mfuko wa PSPF kwa kuja na wazo la kutoa mafunzo kwa viongozi hao kuhusu ujasiriamali kwa kuwa wengi wa wastaafu wakiwemo viongozi hukabiliana na maisha magumu pindi wanapostaafu kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ya namna ya kujipatia kipato kupitia mafao yao.
Aidha, waziri huyo alisema ameagizwa na Rais Magufuli awahakikishie wakuu hao wa wilaya wastaafu kuwa mchakato wa kulipwa mafao yao tayari umeshaanza na muda wowote wataanza kulipwa fedha zao. “Ameniambia niwaambie wazi kuwa uhakika upo, muda si mrefu mambo yatakuwa mazuri.”
Blogger Comment