KUNA vita ya maneno kati ya makundi mawili ya mashabiki wa Muziki wa Bongo Fleva, wanaowashabikia wasanii Alikiba na Nasibu Abdul ‘Diamond’, kila upande ukidai mtu wao ndiye anajua zaidi kuliko mwingine.
Ni mjadala mpana katika mitandao ya kijamii, mitaani na hata miongoni mwa wasanii wenyewe ambao kwa kificho au waziwazi, wamewahi kuzungumzia nani mkali katika wawili hao ambao wote ni vijana wenye asili ya Kigoma.
Alikiba ama King Kiba, ndiye wa kwanza kuingia na kupata jina katika Muziki wa Bongo Fleva, katikati ya miaka ya 2000 akiwa na singo yake ya kwanza, Cinderella ndiyo ilimfungulia milango, kwani alichomoza hadi juu ambako alidumu kwa muda mrefu.
Huenda Diamond amewahi kuimba kwa kuiga baadhi ya nyimbo za Alikiba, kwa sababu yeye alianza kupata jina mwaka 2009, mwaka ambao mwenzake tayari alishakuwa na albamu mtaani.
Unapotaka kufanya ulinganisho wa wawili hawa ni lazima uchague unataka kuwalinganisha nini, vinginevyo unaweza kujikuta umewekeza katika chuki au ushabiki, kitu ambacho hakitakiwi. Kwa mfano, vigumu kupata idadi kamili ya mashabiki wa wasanii hao, ingawa mapokeo ya kazi zao yanaweza kumuongoza mtu kuelewa.
Kitu kimoja cha msingi ambacho wengi wanakubaliana ni kwamba Alikiba ana uwezo mkubwa wa kuimba na mwenye sauti nzuri kuliko Diamond. Msanii mmoja chipukizi, Ibrahim Kidugu ‘Wizzy Rapper’ katika kibao chake cha Kote Nisikike, kwenye mojawapo ya vesi anasema “Ali ni mwanamuziki, Nasibu Mfanyabiashara.”
Maana ya Wizzy Rapper ni kuwa Diamond anafanya biashara ya muziki, ndiyo maana anaonekana kuwa juu ya Alikiba ambaye anafanya muziki kwa mazoea.
Katika ubora wake, Alikiba aliwahi kukutana na mkali wa R&B duniani, R Kelly, katika projekti iliyoitwa One8, ambapo wakali nane wa Afrika walifanya ngoma moja iliyoitwa Hands Across Africa ambao walikuwa ni yeye, Fally Ipupa, 2Face, Amani, Movaizhaleine, 4X4, Navio na JK.
Licha ya Kiba kufika nyumbani kwa R Kelly, studio kwake, alishindwa kutumia ushawishi wa msanii huyo mkubwa ili aweze kumsaidia kuingia katika soko la Marekani. Mbaya zaidi, alishindwa pia kujitangaza kimataifa kupitia Fally Ipupa na 2Face ambao ni maarufu kuliko yeye.
Ambwene Yessaya ‘AY’ alimkutanisha Diamond na Davido wa Nigeria na akafanya naye Ngoma ya Number One Remix. Hapa kijana yule wa Tandale hakutaka kuishia kwa msanii huyo pekee, akaingia nchini humo na kufanya kazi na wasanii karibu wote wakubwa, wakiwemo waliofanikiwa zaidi, P Square.
Hiyo imempa Diamond kujulikana zaidi na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii wakubwa Afrika, kiasi cha wengi kuhitaji kolabo naye kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe, Ivory Coast na kwingineko Afrika.
Alikiba haonekani kuwekeza akili yake yote katika muziki anaoufanya. Ni kama mtu ambaye anafanya muziki kwa kujifurahisha na siyo kufikia malengo ambayo mashabiki wake wangependa aende. Ana uwezo mkubwa nyuma ya Mic, lakini ameshindwa kuutumia ili kuliteka soko.
Kiba anaridhika au labda niseme, mvivu. Katika uhalisia ni makosa kumshindanisha na Diamond kwa sababu haoneshi kama ni mshindani wake. Alipokuwa katika ziara yake Ulaya, akaitumia nafasi adimu aliyoipata kukutana na marehemu Papa Wemba na kufanya naye wimbo.
Baada ya kuliweza soko la Afrika, Diamond anaonekana wazi kulitamani la Ulaya na Marekani na hii ndiyo sababu ya yeye kuwa msanii anayelipwa zaidi kuliko wote kwa sasa hapa Bongo.
Kiba hatafuti kolabo na watu wa nje kwa vile anadhani ataonekana anamuiga mwenzake, wakati katika maisha, kuiga vitu vizuri na vya maendeleo ni jambo la kupongezwa.
Hata hivyo, Kiba anayo nafasi ya kubadilika ili aweze kuwa mshindani wa kweli wa Diamond, vinginevyo asahau.
Blogger Comment