WCB:WASAFI TAA NYEKUNDU HIYOOO!

WCB
BILA shaka ukiambiwa utaje orodha za lebo kubwa za muziki barani Afrika, huwezi kuacha kuitaja WCB inayomilikiwa na mkali Diamond Platinumz wa hapa Bongo.
Kwa mwaka 2016, mbali na Diamond kutoa nyimbo kali, lebo hii imetambulisha wasanii wapya wawili, Harmonize na Raymond.
Mbali na hao, pia WCB pia imefanikiwa kumsainisha Rich Mavoko mkataba wa kusimamia kazi zake.
Ni jambo jema kwa muziki wetu, lakini katika kipindi cha miezi miwili hivi sasa, lebo hii imeachia nyimbo za wasanii wake wote, hali inayofanya wasanii hao kufunikana wenyewe kwa wenyewe.
Menejimenti ya WCB inayosimamia promo nzima za wasanii wake pindi wanapoachia nyimbo ni kama imekosa utaratibu mzuri wa kupanga ni muda gani nani anatakiwa atoke na anahitaji promo ya ukubwa gani kwa kipindi gani.
Kutoka mwezi Mei mpaka Julai mwaka huu, WCB imeachia nyimbo nne za wasanii wao, hali iliyopelekea baadhi ya nyimbo kupotea ama kuchuja haraka.
Zifuatazo ni orodha ya nyimbo nne zilizoachiwa na WCB katika kipindi cha miezi hii miwili, na hapa utabaini namna wakali wa lebo hii wanavyopotezana wenyewe kwa wenyewe bila kujijua.
Natafuta Kiki (Raymond)
Huu ulikuwa wimbo wa kwanza kutoka WCB katika kipindi cha miezi hii  miwili. Baada ya kufanya vyema na wimbo wa ‘Kwetu’, kijana aliyeibuliwa na WCB, Raymond aliachia wimbo huu ukiwa ni wa tatu baada ya ule wa ‘Penzi’ aliomshirikisha Harmonize.
Licha ya uzuri wa mashairi wa ‘Natafuta Kiki’  huwezi kuacha kutaja promo kubwa iliyofanywa na Lebo ya WCB kupitia redio, TV, magazeti na mitandao ya kijamii katika kuhakikisha wimbo huu unafika kwa wingi kwa wananchi, bahati ukafika na ukakubalika.
Ibaki Stori (Rich Mavoko)
Wakati wimbo wa ‘Natafuta Kiki’ ukiendelea kufanya vyema kwenye vituo mbalimbali vya Radio na TV, mwanzoni mwa mwezi wa sita WCB walimsainisha msanii Rich Mavoko na kumuweka chini ya lebo yao.
Saa chache baada ya utambulisho huo, Rich Mavoko chini ya WCB aliachia hewani wimbo na video ya ‘Ibaki Stori’.
Video ya wimbo huu iliyofanyika Afrika Kusini ulipokelewa vyema na mashabiki wa muziki nchini, kitendo kilichofanya nyimbo ya ‘Natafuta Kiki’ ya Raymond ambao ulikuwa hauna video kumezwa na kupotea kabisa.
Matatizo (Harmonize)
Ajabu na kweli, mwezi mmoja baadaye, uongozi wa WCB ukatambulisha tena wimbo na video ya ‘Matatizo’ ulioimbwa na Harmonize.
Wimbo huu ulionekana kuja ghafla sana kinyume na ratiba zilizokuwa zikitangazwa na WCB, hali iliyomfanya mmoja wa viongozi wa lebo hii kubwa nchini kusimama na kueleza kwanini waliamua kuachia kwa haraka wimbo wa ‘Matatizo’.
Katika maelezo yake alieleza kuwa kuchelewa kwa nyimbo mpya ya Diamond ndiyo umewafanya watoe wimbo mpya ili kuwafurahisha mashabiki wao.
Kumbuka wimbo huu wa Harmonize ulitoka wakati mashabiki wakianza kukariri mashairi ya wimbo wa ‘Ibaki Stori’ wa Rich Mavoko.
Kilichotokea ni watu kuusahau wa Mavoko na kuhamisha akili zao kwa Harmonize ambaye naye katika kipindi kifupi kilichopita alikuwa akitamba na wimbo wa ‘Bado’ uliomezwa na ule wa ‘Kwetu’ wa Raymond.
Kidogo (Diamond ft P Square)
Baada ya ukimya wa muda mrefu tangu alipoachia wimbo ya ‘Utanipenda’, bosi wa WCB, Diamond Platinumz aliachia wimbo na video mpya wa ‘Kidogo’ aliowashirikisha wakali kutoka Nigeria, P Square.
Ujio wa wimbo huu uliotoka wiki chache tangu lebo hiyo ilipoachia wimbo wa ‘Matatizo’, umeonekana kuja kuzizima nyimbo zote zilizotolewa na lebo hiyo kutoka mwezi Mei, mwaka huu.
Unajua ni kwanini? Nguvu kubwa ya promo ilielekezwa hapo na kuzifanya nyimbo za ‘Natafuta Kiki’ ‘Ibaki Stori’ na ‘Matatizo’ kupoteza nguvu kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni.
Ushauri wa bure
Wazo la kuwa na lebo ni zuri sana, tena lenye tija lakini lazima kuwepo na mpishano sokoni kati ya wasanii waliopo kwenye lebo ili kuepusha mgongano wa masilahi.
Kutakuwa na maana gani sasa kama wimbo unatolewa leo, unahiti mbaya kitaa, halafu baada ya wiki tatu unatoka wa msanii mwingine katika lebo hiyohiyo?
Katika hili, menejimenti ya WCB inapaswa kutulia na kutafakari kwa kina. Wanaweza kutumia fedha nyingi kwenye promo ya wimbo wa msanii ambaye baadaye wanakuja kuua wimbo wake kwa kazi ya msanii wao mwingine.
Mnayo nafasi ya kujipanga. Si lazima kufuata, ni ushauri wangu kama mdau na mpenda maendeleo ya muziki wa Bongo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment