Msanii Nay wa Mitego ambaye siku za karibuni wimbo wake mpya ‘Pale kati’ umefungiwa na Baraza la sanaa Taifa (BASATA) amefunguka na kusema kuwa suala la watu kusambaza picha kwenye mitandao ya jamii huku zikiwaonyesha wanawake wakiwa hawana nguo kabisa siyo kosa lake yeye kwani hakufanya hicho kitu bali kuna watu walitengeneza hizo picha wakiwa na malengo yao.
Nay wa Mitego amesema hayo katika kipindi cha Planet Bongo ya East Africa Radio na kudai kuwa kuna watu walikuwa wanatengeneza picha hizo na kuzisambaza ila yeye hajafanya hivyo, na kudai kuwa alishajaribu kuwaripoti watu wengine ambao walikuwa wanafanya mchezo huo.
“Suala la picha za wimbo huo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii huku zikionyesha wanawake wakiwa nusu uchi si suala langu mimi, maana dunia ya sasa kuna watu wanafanya ‘editing’ ya picha sana, kama mtakumbuka hata kipindi nimetoa ‘Shika adabu yako’watu walinitengeneza sana kwenye picha na kusambaza kwenye mitandao ya jamii, hivyo suala la picha hilo siyo tatizo langu” alisema Nay wa Mitego.
Mbali na hilo Nay wa Mitego amesema kuwa yeye hajaridhishwa na maamuzi ya BASATA kufungia wimbo wake mpya kwa kigezo cha picha kwani walipaswa kusubiri video itoke ndiyo inaeleza vizuri maana ya wimbo wake huo.
“Huwezi kufungia ‘Audio’ kwa sababu ya picha BASATA walitakiwa kusubiri nitoe video kwani video inatoa tafsiri nzuri ya wimbo huo na kama kungekuwa na tatizo kwenye video ndiyo tulipaswa kukaa na hawa walezi wetu katika muziki BASATA ili kuona tunaweza kurekebisha jambo gani katika video” alimalizia Nay wa Mitego
Blogger Comment