KIONGOZI Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, amemuunga mkono Rais John Magufuli, kwa kuwakataza wafuasi wote wa chama hicho, kutojihusisha na maandamano ya aina yoyote kwa kuwa chama hicho hakijatangaza maandamano.
Kauli hiyo ya Zitto, imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kuonya kuwa atakayethubutu kuandamana atakiona cha mtema kuni, huku Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, akitangaza kuwa maandamano ya wafuasi wa chama hicho nchi nzima, yako pale pale.
Katika taarifa yake aliyotoa jana kwa vyombo vya habari, Zitto amesisitiza kwa wanachama hao na wafuasi wa chama hicho, kutojihusisha na maandamano ya aina yoyote kwa kuwa chama hicho hakijatangaza maandamano.
Kauli hiyo ya Zitto ni pigo lingine kwa Chadema, ambayo juzi kupitia Mwalimu ilidai kupata barua za kuungwa mkono na taasisi nyingi katika maandamano hayo.
Polisi
Mwanzoni mwa Juni mwaka huu, Jeshi la Polisi nchini, kupitia kwa Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, lilipiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, iliyokuwa imepangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya siasa.
Kamishna Mssanzya alisema kuwa jeshi hilo lilipata taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa, vikitaka kufanya mikutano na maandamano, lakini wakapiga marufuku baada ya kubaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.
Baadhi ya vyama hivyo, ilielezwa kuwa vilionesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao, ambapo watafsiri wa mambo walieleza kuwa hali hiyo ilikuwa ijitokeze katika mikutano ya chama tawala na Chadema inayoongoza Ukawa, ambayo yote ilipigwa marufuku.
Msajili
Mbali na Polisi, wiki hii Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alikemea tamko la Chadema lililotolewa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe la kuitisha maandamano hayo, akisema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, maudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Alikumbusha kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 kifungu (2) (c) inakataza chama cha siasa kutumia au kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake kisiasa.
Alisema kifungu cha 9 (2) (f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu wanachama au viongozi wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha kutokea uvunjifu wa amani.
Rais
Katika onyo alilotoa Rais Magufuli, alifafanua kuwa hajapiga marufuku wanasiasa kufanya mikutano ya kuhimiza maendeleo kwenye maeneo yao.
“Kama wewe ni mbunge wa Jimbo la Hai (kwa sasa Freeman Mbowe), zunguka kwenye jimbo lako hadi uchoke, si unaacha kwako unaenda Shinyanga kushawishi watu waandamane. Mimi sijazuia shughuli za waliochaguliwa kwenye maeneo yao, bali nimekataa mtu kuondoka jimboni kwake na kwenda kufanya fujo mahali pengine. “Wengine nikitoa maamuzi hayo, wanabadilisha maneno, walizoea vitu vya kubembelezana bembelezana, wanasema tunaandamana unambembeleza?, Kaandamane ukione,” alikaririwa akisema.
Maelezo zaidi ya Zitto
Katika hatua nyingine Zitto amewataka wafuasi hao, kutoona aibu kuunga mkono uamuzi wowote wa serikali au chama chochote cha siasa, unaoendana na azimio la Tabora hususan katika vita dhidi ya ufisadi na kurejeshwa kwa miiko ya uongozi.
“Tuwe mstari wa mbele kupinga ufisadi kwani rushwa ni adui wa haki. Tuwe mstari wa mbele kutaka kurejeshwa kwenye miiko ya uongozi, sisi ndiyo chama pekee chenye itikadi iliyo wazi, tuisimamie popote tulipo bila woga wala aibu,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika taarifa yake hiyo, Zitto amewataka wanachama wa chama hicho kusoma, kuelewa na kujadili Azimio la Tabora na kuchambua muktadha wake katika mazingira ya sasa ya siasa za nchini, kwa kuwa chama hicho kiliundwa kwa madhumuni ya kurejesha nchi kwenye misingi yake.
Kuandika barua
Aidha, ameagiza kila mwanachama wa chama chake aandike barua kwa Rais Magufuli kwa namna anavyoona yeye kumtaka alichodai kuacha kuingiza nchi kwenye utawala wa imla.
“Chama chetu kina wanachama 431,120 wenye kadi, Ikulu ikipata barua 200,000 kutoka kila kona ya nchi itafunguka macho,” ilidai taarifa hiyo.
Blogger Comment