WAFANYABIASHARA wawili, akiwemo Mohamed Yusufali “Choma”, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka 222 ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 14.
Mbali na Yusufali aliyewahi kutajwa kuwa anajipatia Sh milioni saba kwa dakika moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali, mshitakiwa mwingine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Limited, Samwel Lema, ambao wanadaiwa kusababisha hasara kwa kughushi na kukwepa kulipa kodi.
Washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka kwa zaidi ya saa tatu na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi, akisaidiwa na Jackline Nyantori, Diana Lukondo na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri, ilidaiwa, katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi 2012 na Desemba 31, 2014, washitakiwa hao na wengine ambao hawajafikishwa mahakamani walipanga njama za kuidanganya Mamlaka ya Mapato (TRA) na kujipatia Sh 14,052,011,435.
Wakili Kishenyi akisaidiwa na Nyantori walidai, katika shitaka la tano hadi 103 kuwa, kati ya mwaka 2011 na 2013, jijini Dar es Salaam na Arusha, washitakiwa hao walighushi stakabadhi za malipo kuonesha Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd imenunua bidhaa mbalimbali.
Ilidaiwa kuwa stakabadhi hizo zilionesha kuwa kampuni hiyo imenunua bidhaa mbalimbali kutoka kwenye kampuni tofauti tofauti ikiwemo ya Festive General Business Ltd, Ever Global General Trading na Jambo Product Ltd, jambo ambalo si kweli.
Wakili Diana na Swai waliendelea kudai, katika shitaka la 104 hadi 141, kuwa kati ya mwaka 2011 na 2015, Lema alighushi hati ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuonesha kuwa kampuni yake imenunua bidhaa mbalimbali kutoka kampuni tofauti tofauti ikiwemo ununuzi wa vifaa vya Sh bilioni 1.7.
Wakili Swai alidai katika shitaka la 142 hadi 219 kuwa, kwa lengo la kufanya udanganyifu washitakiwa hao walighushi stakabadhi za malipo kuonesha Kampuni ya Elerai Constructions Ltd, imenunua vifaa mbalimbali kutoka katika kampuni tofauti tofauti ikiwemo Kampuni ya Blue Arrow Tanzania Ltd.
Aliendelea kudai shitaka la 220, linamkabili Lema ambaye anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2012 na Desemba 31, 2015, Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi anayehusika kushughulikia Kampuni yake ya Northern Engineering Works Ltd na Elerai Constructions Ltd zilizosajiliwa kama walipa kodi, aliwasilisha nyaraka za uongo.
Inadaiwa aliwasilisha nyaraka ambazo ni marejesho ya uongo ya Kodi ya VAT kwa Kamishna Mkuu wa TRA jambo lililosababisha akwepe kulipa kodi ya Sh bilioni 14,052,011,435.
Katika mashitaka ya utakatishaji wa fedha, ilidaiwa kati ya Februari Mosi, 2012 na Februari 25, 2013 jijini Dar es Salaam na Arusha, washitakiwa hao walijihusisha na kuhamisha Sh milioni 420 zilizotokana na vitendo vya uhalifu.
Inadaiwa waliziingiza fedha hizo kwenye akaunti namba 1010000541 inayomilikiwa na Iqbal Jaferali Jafferjee iliyopo katika Benki ya I&M tawi la Kariakoo, na kuzitoa huku wakijua zimepatikana kwa njia za uhalifu ambazo ni kughushi na kukwepa kulipa kodi.
Iliendelea kudaiwa katika shitaka la 222 kuwa, kati ya Januari Mosi, 2012 na Desemba 31, 2015, Dar es salaam, kutokana na vitendo vyao vya kuwasilisha marejesho ya VAT ya uongo kwa Kamishna Mkuu wa TRA waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh bilioni 14.
Hakimu Mashauri aliwaeleza washitakiwa hao kuwa, hawaruhusiwi kujibu mashitaka yao kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu.
Baada ya kusomewa mashitaka, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa, hata hivyo Wakili Alex Mgongolwa anayeongoza jopo la Mawakili wa Utetezi aliomba kuwasilisha ombi.
Aliiomba Mahakama ifute shitaka la utakatishaji wa fedha kwa kuwa lina mapungufu makubwa ya kisheria ambayo hayawezi kurekebishwa wala kufumbiwa macho isipokuwa kufutwa.
Alidai ili shitaka liwe la utakatishaji wa fedha lazima kuwa na dhamira ya kuficha chanzo cha fedha au lengo la washitakiwa kukwepa adhabu lakini kama hakuna mambo hayo sheria inatoa mamlaka kwa Mahakama kuyafuta mashitaka hayo.
Upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo ili wajiandae kujibu hoja za upande wa utetezi. Hakimu Mashauri alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kusikiliza majibu ya Jamhuri.
Washitakiwa wote walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana. Mbali na mashitaka hayo, Choma anakabiliwa na kesi nyingine yenye mashitaka 199 ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6 katika mahakama hiyo.
Blogger Comment